Friday, March 25, 2011

MAREHEMU FIVE STARS MODERN TAARAB WAOMBEWA DUA

   Naibu Waziri wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Dtk.Fenela Mukangala akiongea na waumini pia wadau wa Sanaa waliofika katika Ukumbi wa Star Light Ilala jijini Dar es Salaam kuwaombea dua maalum Marehemu 13 wa Kundi la Five Star Modern Taarab waliofariki katika ajali iliyotokea wiki hii kwenye barabara ya  Iringa-Morogoro.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni,Sanaa kutoka wizara hiyo,Bi.Ngowi.
Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni Prof.Hermans Mwansoko naye akiongea jambo katika dua hiyo maalum ya kuwaombea marehemu.Wengine kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Ghonche Materego na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga,Mh.Henry Clemensia.
                                       Waumini wakiomba dua kwa marehemu
Mmoja ya Wasanii waliopona kwenye ajali hiyo Ally Juma aka Ally J (Kulia) akiwa sambamba na Viongozi wa Bendi yake, Ferouz Juma (wa pili kutoka kulia) Mkurugenzi wa Bendi ya Five Star na Khamis Slim (Wa kwanza kushoto) ambaye ni Mwenyekiti wa Bendi.

Baadhi ya wasanii wa taarab wakisikiliza mawaidha kutoka kwa Sheikh Othman Zuberi (hayuko pichani) wakati wa dua hiyo.
Mratibu wa shughuli ya kuwaombea dua Marehemu,Mzee Chilo akitangaza utaratibu mbalimbali wa tukio zima.
Shirikisho la Wasanii Tanzania (SHIWATA) Alhamisi ya wiki hii kwenye Ukumbi wa Star Light Ilala jijini Dar es Salaam liliandaa dua maalum ya kuwaombea wasanii 13 wa Kundi la Five Stars Modern Taarab waliofariki Dunia usiku wa Tarehe 21/3/2011 kutokana na ajali ya gari iliyotokea eneo la Hifadhi ya Wanyama ya Mikumi mkoani Morogoro.
Dua hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa,mashirika ya umma, masheikh, wachungaji na wasanii mbalimbali hususan wa taarab.
Miongoni mwa waliohudhuria dua hiyo maalum ya kuwaombea marehemu ni Naibu Waziri wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Mh.Dtk.Fenela Mkangala,Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni kutoka wizara hiyo,Profesa Hermans Mwansoko,Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni anayeshughulikia Sanaa,Bi.Angela Ngowi,Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh.Henry Clemensia.
Akizungumza katika Dua hiyo,Naibu Waziri wa Wizara ya Habari,Dkt.Mukangala alisema kwamba,kifo cha wasanii hao ni pigo kubwa katika tasnia ya Sanaa lakini lazima wadau wa sanaa wajipange kuhakikisha kundi la Five Star linarudi katika hali yake na kuwa bora zaidi.
“Serikali itakuwa bega kwa bega katika  kutoa ushirikiano wa dhati kwa kundi la Five Star kupitia idara yetu ya Utamaduni.Ni wajibu wa wadau wote wa sanaa kulisaidia kundi kwani katika ajali hiyo si tu lilipoteza wasanii hao 13 bali pia vyombo karibu vyote vya muziki” alisisitiza Dkt.Mukangala.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga,Mh.Clemensia aliwaasa wasanii kutunga nyimbo za kukemea madereva wanaoendesha magari yao kwa kasi na wasio zingatia sheria za barabarani.Aidha, alikiri kwamba, pengo la wasanii hao wa kundi la Five Stars haliwezi kuzibika kamwe kutokana na ukweli kwamba,kazi yao haina mbadala.
Awali kabla ya wageni kuzungumza,Sheikh Othman Zuberi aliongoza dua maalum ya kuwaombea marehemu ambapo naye hakusita kuasa juu ya wasanii kuzingatia maadili na kuvaa mavazi yanayo wasitiri badala ya kutumbukia kwenye mtego wa kutenda maovu kupitia kazi zao za sanaa.

 

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU