Thursday, March 24, 2011

KAMATI YA MASHINDANO

Kamati ya Mashindano chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Ramadhan Nassib ilikutana Machi 19 mwaka huu na kupitia taarifa za mashindano mbalimbali. Miongoni mwa matukio yaliyoripotiwa na waamuzi na makamishna yaliyofikishwa kwenye kamati hiyo yalihusu mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
Mechi namba 86 kati ya Majimaji na Yanga iliyochezwa Februari 5 mjini Songea, ripoti ilionesha kuwa wachezaji wa Yanga walivunja viti katika Uwanja wa Majimaji, kuvunja mlango wa Mama Lishe na washabiki wake kutaka kuvamia waamuzi baada ya mchezo.
Kocha wa Toto African, Choke Abeid alimtukana mwamuzi wa mezani matusi ya nguoni na kutupa chupa ya maji chini katika mechi namba 95 dhidi ya Simba iliyochezwa CCM Kirumba, Mwanza. Kwa kitendo hicho mwamuzi alimuondoa kwenye benchi la wachezaji.

Katika mechi namba 96 iliyochezwa Bukoba kati ya Kagera Sugar na Yanga, wachezaji wa Kagera, Msafiri Devo na David Luhende waliwarushia waamuzi chupa za maji na kutoa matusi ya nguoni.

Naye kipa wa Mtibwa Sugar, Shabani Kado ameripotiwa kumtukana matusi ya nguoni mwamuzi kwenye mechi namba 103 dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Mwanza ambapo alitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Licha ya kanuni kueleza adhabu kwa makosa hayo, kujirudia mara kwa mara na mengine kufanyika nje ya uwanja, Kamati ya Mashindano imeyaandikia taarifa na kuyawasilisha kwenye Kamati ya Nidhamu ikipendekeza adhabu zaidi kwa wahusika.

U23 KUONDOKA MACHI 24

Msafara wa timu ya U23 wenye wachezaji 18 kwenda Cameroon utaondoka Machi 24 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Athuman Kambi.

Wachezaji hao ambao wako chini ya Kocha Jamhuri Kihwelo na msaidizi wake Ayoub Mohamed ni Jamal Mnyate, Salum Telela, Omega Seme, Mussa Gharib, Cosmas Lewis, Abdulrahim Shaaban, Zahoro Pazi, Issa Rashid, Himid Mao, Salum Abubakar, Mcha Khamis, Amour Suleiman, Samuel Ngasa, Shomari Kapombe, Babu Ally, Bakari Hamis, Faraji Kabali na Thomas Ulimwengu.

Wengine kwenye msafara huo ni Meneja wa Timu, Mohamed Rishard, Daktari wa Timu, Dk. Joachim Mshanga na mtunza vifaa (Kit Manager), Edward Venance.

MECHI YA SIMBA v KAGERA SUGAR

Mchezo namba 122 wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera Sugar uliokuwa uchezwe Machi 27 mwaka huu Uwanja wa Uhuru umesogezwa mbele kwa siku moja na sasa utafanyika Machi 28 mwaka huu.
Mchezo huo umesogezwa ili kutoa fursa kwa wachezaji watano wa Simba walioko Taifa Stars kujiunga na timu yao baada ya mechi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati itakayochezwa Machi 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.








0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU