Thursday, June 2, 2011

KUTOKA TFF


Mechi ya kwanza ya mchujo ya michuano ya Olimpiki kati ya timu ya Taifa ya
Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23 dhidi ya Nigeria itafanyika
Jumapili (Juni 5, 2011) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 kamili
jioni.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 1,000 kwa viti vya kijani, bluu na
rangi ya chungwa (orange straight and curve), sh. 5,000 kwa VIP C na B na sh.
10,000 kwa VIP A. Tiketi zitaanza kuuzwa Ijumaa saa 2 asubuhi kwenye vituo vya
Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa, Bigbon Msimbazi (Kariakoo), Steers (Mtaa wa
Ohio na Samora), Uwanja wa Uhuru, Ubungo OilCom na vituo vya mauzo vya Premier
Sports Betting.

Nigeria itawasili Juni 3 mwaka huu kama ilivyo kwa waamuzi wa mechi hiyo kutoka
Kenya na Kamishna kutoka Ethiopia. Mwamuzi ni Sylvester Kirwa ambaye atasaidiwa
na Peter Kiereini, Aden Marwa na Davies Omweno wakati Kamishna ni Sahilu
Gebremariam.

Pia TFF kupitia Kurugenzi ya Masoko imepiga marufuku wachuuzi wa viburudisho
kwenye mechi hiyo, isipokuwa kwa kampuni maalumu iliyopewa kazi hiyo. Hivyo
vijana wote watakaofanya biashara bila kibali cha TFF watakamatwa. Suala hili
pia linawahusu wachuuzi wa jezi za timu ya Taifa uwanjani.

KALENDA YA MATUKIO.

TFF imetoa kalenda yake ya matukio kwa mwaka 2011/2012 ambapo kipindi cha kwanza
cha matayarisho ya msimu kinaanza Juni 1 hadi Agosti 13 mwaka huu. Kipindi cha
kwanza cha uhamisho kinaanza Juni 1 hadi Julai 15 ambapo usajili wa kwanza
utakuwa Juni 1 hadi Julai 20.

Kutangaza wachezaji wa kuachwa/kusitisha mikataba ni kuanzia Juni 1 hadi 21
mwaka huu wakati kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Julai 21-31
mwaka huu.

Kipindi cha pili cha uhamisho kitaanza Novemba 1 hadi 20 mwaka huu wakati
usajili utaanza Novemba 1 hadi 30 mwaka huu. Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom
inatarajiwa kutoka Julai 20 mwaka huu. Ngao ya Hisani kwa ajili ya ufunguzi wa
msimu kwa mikoa yote itachezwa Agosti 13 mwaka huu wakati mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu ya Vodacom utaanza Agosti 20 mwaka huu.

TFF tunawaomba wadau wote kuhakikisha wanapata kalenda hii ili waweze kupanga
shughuli na mipango yao kwa kuizingatia.

WACHEZAJI MRWANDA, KASSIM.

Dan Mrwanda na Abdi Kassim ni miongoni wa wachezaji saba wanaocheza mpira wa
kulipwa nje ya nchi walioitwa na kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen kwa ajili ya
mechi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati itakayofanyika Juni 5 mwaka huu jijini
Bangui.

Klabu yao ya Dong Tam Long ya Vietnam imekataa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga
na Stars kwa madai kuwa iko kwenye hali ngumu katika ligi yao. Timu hiyo
inashika nafasi ya mwisho kwenye ligi ya nchi hiyo inayoshirikisha timu 14,
hivyo kudai kuwa wachezaji hao ni muhimu kwao kuwaokoa kutoka mkiani.

TFF tumepinga hatua hiyo kwa vile ni kinyume na Kanuni ya Hadhi na Uhamisho wa
Wachezaji (Regulations of Status and Players Transfer), hivyo tutawasilisha
malalamiko yetu kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

KOZI YA WAKUFUNZI WA WAAMUZI

Kozi ya Wakufunzi (Instructors) wa Waamuzi wa Mikoa imeanza leo (Juni Mosi)
jijini Dar es Salaam ikishirikisha wakufunzi 16 kutoka mikoa mbalimbali ya
Tanzania Bara.

Wawezeshaji katika kozi hiyo itakayomalizika Juni 4 mwaka huu na inayofanyika
Ofisi za TFF ni Hafidh Ally, Leslie Liunda, Joseph Mapunda, Riziki Majala na
Juma Ali David.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU