Thursday, June 9, 2011

TIMU YA VILLA SQUAD KUFANYA UCHAGUZI JUNI 12 MWAKA HUU

KLABU ya Villa Squad ya Kinondoni, Dar es Salaam, inatarajiwa kufanya uchaguzi Jumapili ya Juni 12, mwaka huu-huku mgombea ujumbe wakati ya utendaji, Ally Ahmad Kindoile, akisema: “Wanachama wasifanye makosa.”
Kindoile ndiye aliyekuwa akiisimamia timu hiyo jijini Tanga ilipokuwa katika harakati za kupanda Ligi Kuu, alisema kwamba uongozi bora ndio utakaoipa mafanikio Villa Squad.
Alisema kwamba timu hiyo ilishuka daraja misimu mitatu iliyopita kwa sababu ya uongozi mbovu na kurejea kwake kwenye ligi hiyo ilikuwa ni baada ya kujipanga upya.
“Sasa tumejipanga na Jumapili tunatarajia kuwa na uchaguzi. Sasa wito wangu kwa wanachama ni kwamba wasifanye makosa. Wanachama wanajua waliohangaika na timu, wanajua watu wanavyowajibika, sasa wasirudie makosa ya miaka ile,” alisema Kindoile.
Katika uchaguzi huo ambao utahitaji kupatikana kwa mwenyekiti, makamu mwenyekitio na wajumbe saba wa kamati ya utendaji, Kindoile anapambana na akina Mohammed Kimbengele, Alwan Mahamoud, Ally Mpemba, Said Chacha, Mohammed Buda na Ramadhani Sudi.
Nafasi ya mwenyekiti kuna mwanachama mmoja tu aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo ambaye ni Abdallah Bulembo, wakati wanaowania nafasi ya makamu ni Idd Mbonde na Ramadhani Uledi.
Akijibu swali la kutowania nafasi za juu, Kindoile alisema: “Sababu kubwa ni mfumo wa uongozi na uwajibikaji. Katika mfumo, nimeona bora niwe kwanza mjumbe kabla ya kupanda huko juu.

“Nafasi za juu naamini zinataka sifa nyingi tu ikiwa ni pamoja na uzoefu na uwajibikaji, nimeona nipate muda wa kujifunza kwanza. Nadhani ni wakati wangu wa kuitumikia Villa Squad vizuri nikianzia ngazi hii ya sasa ya ujumbe,” alisema.
Alisema kwamba hata wadau waliomuomba kuwania uongozi, pia walipendekeza awanie ujumbe kwani wana malengo ya kuweka uongozi ambao siku moja, timu hiyo itatangaza ubingwa wa Bara kutokana na uongozi bora.
Anasema kwamba wataweza kuiweka Villa Squad kwenye ramani nzuri ya soka kwa sababu “Kinondoni ni wilaya ambayo wakubwa wote wanalala hata kama wanafanya kazi Ilala.”
Anakiri kwamba ushindani ni mkubwa kwenye nafasi hiyo, kwa kuwa wanachama wengi wamejiunga na hawafahamu vema viongozi wanaowania uongozi. Villa sasa inakaribia kuwa na wanachama 500.
Alipotakiwa atoboe siri ya kuipandisha Villa Squad, Kindoile anasema: “Ushirikiano uliokuwako baina ya viongozi, wachezaji na mashabiki ilikuwa karata dume kwetu.
“Kulikuwa na timu ambazo ni kama ziliandaliwa kuchukua nafasi ya kupanda, lakini tulipambana na silaha yetu ilikuwa ni ushirikiano na mshikamano ambao sasa nataka utumike katika uongozi huu mpya wa Villa,” alisisitiza.
“Nawashukuru wadau mbalimbali akiwamo Bulembo kwa mchango wa mawazo na fedha kufanikisha kupanda na sasa ni nafasi yetu kufanya kweli,” alisema.



0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU