Wednesday, June 8, 2011

WASAMBAZAJI WATAJWA KUDIDIMIZA SEKTA YA SANAA

Msanii wa muziki na mtafiti wa masuala ya sanaa nchini,Innocent Nganyagwa maarufu kama Ras Ino akizungumza na wadau wa sanaa wakati akiwasilisha mada kuhusu Ubora wa Tungo Katika Kazi za Sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu katika Ukumbi wa BASATA.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,Mafunzo na Habari,BASATA Bw.Godfrey Mungereza.
Mratibu wa Jukwaa la Sanaa Bw.Ruyembe Mulimba akichochea mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.Kulia kwake ni Ras Ino.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,Mafunzo na Habari,BASATA Bw.Godfrey Mungereza akisisitiza jambo wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA.Kulia anayemsikiliza kwa makini ni Innocent Nganyagwa
 
Na Mwandhishi Wetu.

Wasambazaji wa kazi za sanaa nchini wametajwa kuwa chanzo cha kudidimia kwa vipaji vya wasanii nchini kutokana na kuendekeza faida katika kuuza kazi za wasanii pasipo kuzingatia maudhui na ubora wa kazi zao.

Hayo yamesemwa wiki hii na msanii pia mtafiti wa masuala ya sanaa nchini Innocent Nganyagwa wakati akizungumza na wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu ndani ya Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Alisema kwamba,wasambazaji wa kazi za sanaa wamekuwa wakijikita kwenye kuwaahidi wasaniii fedha na magari ili watoe albam au kazi za sanaa bila kuzingatia ubora na maudhui hali ambayo imekuwa ikisababisha kazi hizo zikose ubora na maadili ndani yake.

“Zamani wakati sanaa ni ridhaa,kazi za sanaa zilikuwa na weledi na zenye tungo zilizotukuka ndani yake lakini siku hizi weledi umepotea,wasanii wakishaahidiwa gari na milioni tatu na wafanyabiashara basi atalipua kazi haraka ili iingie sokoni.Hapa tutapata tungo bora?” Alihoji Nganyagwa.

Aliongeza kwamba,uwepo wa nyimbo za taifa na uzalendo vilisaidia sana upatikanaji wa tungo za sanaa zilizotukuka na halisi tofauti na sasa ambapo wasanii wamekuwa ni wa kuiga kila kitu pasipo kuzingatia uhalisia wa mazingira kutokana msukumo wa fedha.

Alihitimisha kwa kutoa wito kwa wasanii kuzingatia weledi katika kazi za sanaa na kuhakikisha wanatafuta msaada huo kila inapobidi kwani wataalam wapo.Aliwataka kuacha kufanya kazi za sanaa kwa kusukumwa na fedha bila kuzingatia uhalisia.
 

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU