Friday, March 15, 2013

TFF YAONDOA ‘FREE PASS’ MPIRANI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeondoa utaratibu wa wadau wake kuingia bure kwenye mechi kwa kutumia tiketi maalum (free pass).

Kutokana na uamuzi huo hakutakuwa tena na pasi za bure kwa ajili ya kushuhudia mechi zilizo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa TFF katika viwanja mbalimbali nchini.

Uamuzi huo umetokana na ukweli kuwa free pass zimekuwa zikipunguza au kuchukua mgawo wote wa TFF kwenye mechi, na wakati mwingine Shirikisho hulazimika kutoa fedha za ziada kugharamia pasi hizo.

Pasi zote ambazo imekuwa ikitoa kwa wadau wake hukatwa katika mgawo wa TFF katika mechi husika. Shirikisho hivi sasa linapata asilimia nne tu ya mapato katika mechi za Ligi Kuu, ligi ambayo hivi sasa inaendeshwa na Kamati yake ya Ligi.

RAMBIRAMBI MSIBA WA OFISA HABARI CECAFA
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa Ofisa Habari wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Finny Muyeshi kilichotokea juzi (Machi 13 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Muyeshi aliitumikia CECAFA kwa muda mrefu, hasa katika kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mazingira mazuri ya kufanyia kazi wakati wanaporipoti matukio mbalimbali ya Baraza hilo.

Alitoa mchango mkubwa katika eneo la habari za mpira wa miguu, tangu akiwa gazeti la East African Standard la Kenya akiwa mwandishi, na baadaye Mhariri wa Michezo kabla ya kujiunga na CECAFA, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Muyeshi, CECAFA, Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) na tasnia ya habari kwa ujumla, na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Muyeshi mahali pema peponi. Amina

FDL KUKAMILISHA MSIMU WIKIENDI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 unamalizika wikiendi hii huku timu za Mbeya City ya Mbeya, Ashanti United ya Dar es Salaam na Rhino Rangers ya Tabora zikiwa tayari zimepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao.

Kundi A mechi zote zitachezwa Jumapili (Machi 17 mwaka huu) ambapo Majimaji vs Mbeya City kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Kurugenzi vs Mkamba Rangers (Mafinga) na Burkina Faso vs JKT Mlale (Jamhuri, Morogoro).

Kesho (Machi 16 mwaka huu) katika kundi B itakuwa Green Warriors vs Polisi Dar (Karume, Dar es Salaam) na Ndanda vs Villa Squad (Nangwanda Sijaona, Mtwara). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Moro United vs Ashanti United (Karume, Dar es Salaam) na Tranist Camp vs Tessema (Mabatini, Mlandizi).

Kundi C ni kesho (Machi 16 mwaka huu) Polisi Tabora vs Pamba (Ali Hassan Mwinyi, Tabora). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Polisi Mara vs JKT Kanembwa (Karume, Musoma), Polisi Dodoma vs Mwadui (Jamhuri, Dodoma) na Rhino Rangers vs Morani (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU