Monday, December 13, 2010

KIKAO CHA NNE CHA SEKTA YA UTAMADUNI CHAFANYIKA MKOANI MWANZA






Kikao cha nane cha sekta ya Utamaduni kimeanza jijini Mwanza kikiwashirikisha wakurugenzi wa idara,maafisa utamaduni wote nchini na wadau mbalimbali wa utamaduni ambapo pamoja na mambo mengine kinatazamiwa kupata taarifa ya hali ya sekta hiyo hapa nchini na kuja na mikakati mbalimbali ya uboreshaji.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuanza kwa kikao,Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni,Profesa Hermans Mwansoko alisema kwamba,kikao hiki kinachobeba kaulimbiu ya Sanaa ni Ajira Tuithamini, kitajikita kwenye uwasilishaji wa mada na machapisho mbalimbali kuhusu sekta ya utamaduni ambapo wajumbe watapata fursa ya kujadili, kuja na changamoto mbalimbali na baadaye kupata majibu na dira ya changamoto hizo.

Aliongeza kwamba,sekta ya utamaduni kwa sasa inakua kwa kasi hivyo, nguvu kubwa lazima iwekezwe huko ili kuhakikisha sekta hii inakuwa chanzo kikubwa cha ajira na mapato miongoni mwa watanzania ikiwa ni pamoja na kulitambulisha taifa katika ngazi mbalimbali za kimataifa.

“Utamaduni ni sekta muhimu nchini,serikali kwa sasa imeweka nguvu katika kuajiri maafisa utamaduni na kuwapandisha hadhi wale waliokuwa wakikaimu ili kuhakikisha sekta hii inakua kwa kasi na kuwanufaisha watanzania na taifa kwa ujumla” alisisitiza Profesa Mwansoko.

Awali akizungumzia kikao hicho,Mratibu wake Michael Kagondera alisema kwamba, kitadumu kwa siku sita ambapo jumla ya mada saba zitawasilishwa,kuchambuliwa na kujadiliwa ikiwa ni pamoja na kujadili mpango mkakati wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wa mwaka 2011-2014 ambao ndani yake umebeba mikakati mingi katika mapinduzi kwenye tasnia ya sanaa nchini.

Mada zitakazowasilishwa ni pamoja na;Nafasi ya Sanaa Katika Ajira nchini Tanzania, Ukuaji wa Tasnia ya Filamu Chachu Katika  Kukuza Ajira, Sanaa Endelevu ni Ujasiriamali, Umuhimu wa Mafunzo Katika Ajira ya Sanaa,Mchango wa Utunzaji Kumbukumbu Katika Kukuza Utamaduni wa mtanzania na ile ya Uzoefu wa Kazi mikoani.

Aidha,katika kikao hiki wasanii mbalimbali waliopata mafanikio kutokana na kuthamini utamaduni wa mtanzania na kufanya sanaa zenye asili ya kitanzania wanatazamiwa kutoa ushuhuda wa zmafanikio mbalimbali waliyoyapata.

Kikao hiki cha cha nane cha utamaduni kitafunguliwa rasmi kesho Desemba 14, 2010 (Jumanne) na Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Dkt Emmanuel Nchimbi.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU