Friday, December 24, 2010

TAARIFA MAALUM KWA WANANCHI


SIKUKUU NJEMA ZA MWISHONI MWA MWAKA ZENYE BURUDANI SALAMA
Hivi sasa tunaingia katika mfululizo wa sherehe za kufunga mwaka 2010 yaani sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya. Tunapojiandaa kufanya hivyo hatuna budi kukumbushana kwamba tunatakiwa kuandaa burudani ambazo ni salama kwa kila mtu na hasa kwa watoto wetu.

Kwa mara kadhaa tumeshuhudia watoto wakiteketea katika burudani za watoto nyakati za Sikukuu. Ikumbukwe kwamba tunawapenda watoto wetu wapate haki yao ya kuburudika lakini pia wawe salama.  

Kwa mara nyingine Serikali inakumbusha mamlaka zote zinazohusika na suala la usalama katika burudani kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa katika kumbi za sanaa na burudani. Maofisa Utamaduni wasitoe vibali vya TOTO DISCO kwa kumbi ambazo siyo salama.

Aidha wenye kumbi wazingatie ujazo wa kumbi zao pasipo kufanya tamaa ya kurundika watu zaidi ya kiwango cha ukumbi na kumaliza shughuli za watoto si zaidi ya saa 12 jioni . 

Wazazi wawe waangalifu katika kuchagua na kuwaongoza watoto wao kwenda mahali ambapo ni salama. Maofisa usalama wasaidie kufuatilia na kusimamia usalama wa raia hasa watoto katika burudani zao.

Ikumbukwe kadri ya taarifa ya Serikali iliyotolewa tarehe 20/09/2010 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw Seth Kamuhanda  kumbi zote zinatakiwa ziwe zimesajiliwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kabla ya tarehe 31 Desemba 2010.
Usajili huu unaendana na marekebisho ya kumbi kulingana na vigezo vya ukumbi salama ambavyo vimesambazwa na BASATA kwa wahusika. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye kaidi agizo hili.

Baraza la Sanaa la Taifa linawatakia wananchi wote na hasa watoto burudani njema katika kuufunga mwaka 2010 kwa hali tulivu, starehe, amani na salama.   

Ghonche Materego
KATIBU MTENDAJI

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU