Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),Ghonche Materego amesema kwamba zoezi la usajili wa wadau wa sanaa linaloendelea nchini kote ni mwanzo wa kujenga heshima ya tasnia ya sanaa ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikionekana kama ridhaa, isiyo na mchango wowote katika uchumi wa nchi na zaidi ya burudani tu.
Akizungumza kwenye Kikao cha nane cha sekta ya Utamaduni kinachofanyika jijini Mwanza.Materego alisema kwamba, ni vema wasanii, wamiliki wa kumbi za sanaa na utamaduni na wadau wote wanaojihusisha na sekta ya sanaa kujisajili na kuwa rasmi kwani wamekuwa kwa muda mrefu wakitengwa na watengeneza sera kutokana na mchango wao kutokuwa ukionekana moja kwa moja.
“Usajili ni hatua ya kwanza ya kuifanya sekta ya sanaa kuwa rasmi na kuheshimika.Ni
lazima wadau wa sanaa wote kwa pamoja tulione hili na kulipa msukumo wa pekee.Kwa muda mrefu watengeneza sera wa nchi yetu wamekuwa wakishindwa kutujumuisha kwenye masuala mbalimbali ya kimataifa na ya maendeleo yetu wenyewe,hili lazima lifike mwisho” alilisisitiza Materego.
Kuhusu gharama za usajili,Materego alisema kwamba, ni nafuu na zinazoweza kulipwa na wadau wote wa sanaa wakiwemo wasanii kwani vimewekwa kwa mujibu wa sheria ndogo za BASATA ambazo ziliwekwa kwenye gazeti la serikali na kuthibitishwa na wizara baada ya kuonekana vinakidhi.
Kwa mujibu wa viwango vya usajili vya BASATA vilivyopo,usajili unagharimu shilingi elfu thelathini huku zile za vibali zikitofautiana kulingana na wadau husika.
0 maoni:
Post a Comment