Monday, February 21, 2011

WAKE WA VIONGOZI WATOA MSAADA WA SH. 1.5M/-



MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda leo mchana (Jumatatu, Februari 21, 2011) amewaongoza wake wa viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoa msaada kwa watu waliopata maafa kutokana na mlipuko wa mabomu ya Gongo la Mboto, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam. 

Akitoa taarifa kwa niaba ya akinamama hao 26 walioambatana naye, Mama Pinda alisema wao kwa niaba ya wake wengine wa viongozi ambao wameshindwa kufika kutokana na majukumu mengine, wameguswa na tukio hilo na wanawapa pole waathirika wote kwa maafa yaliyowapata.

“Tunatambua kuwa kuwa wako waliofariki, waliopoteza wapendwa wao na waliopata ulemavu na wengine waliopoteza mali katika tukio hili... wote tunawapa pole na kumuomba Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,“ alisema.

Alisema wanatoa pole kwa wote lakini zaidi kwa akinamama kwa sababu wao ndiyo wanahangaika zaidi majanga yanapotokea ikiwemo kukimbia na watoto au ndugu wasiojiweza.

Misaada iliyotolewa ni kilo 200 za mchele, kilo 100 za sukari, kilo 500 za unga wa mahindi, mafuta ya kujipaka katoni moja, sabuni za kufulia katoni moja, dawa za meno katoni moja, doti za khanga 55 ambayo ina thamani ya sh. milioni 1.5/-. Pia walitoa mabegi matatu ya nguo za wakubwa na watoto ambazo thamani yake haikuweza kupatikana mara moja.

Akipokea misaada hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Meck Sadick, aliwashukuru viongozi hao na kuwaahidi kuwa itakabidhiwa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ambayo itavigawa vifaa hivyo kwa wahusika.

Wake hao wa viongozi walitembelea pia Hospitali ya Wilaya ya Temeke ambako Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Mariam Malliwa aliwaeleza kwamba hivi sasa wamebaki wagonjwa wawili tu ambao wanaendelea vizuri. Alisema mlipuko ulipotokea walipokea wagonjwa 139, ambao sita walipelekwa Muhimbili, 129 walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani lakini wawili walifariki.

Pia walikwenda Hospitali ya Amana ambayo ni Hospitali ya Wilaya ya Ilala ambako walitembelea wodi ya watoto, wodi ya wanaume na wodi ya akinamama wajawazito ambako walimkuta Bi. Anze E. Jimmy (25) aliyefanyiwa upasuaji kutokana na mshtuko wa mabomu. Bi Anze amepata watoto watatu ambao hadi sasa wako katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uangalizi zaidi na yeye bado yuko Amana kwa sababu amezinduka hivi karibuni.

Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa wa Dharura, Dk. Christopher Mnzava aliwaeleza kwamba tangu mlipuko wa mabomu utokee, wamepokea wagonjwa 263 ambao kati yao 81 walilazwa, 35 walipelekwa Muhimbili na waliobaki walitibiwa na kuruhusiwa. Hivi sasa wamebakia 21 wagonjwa tu.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU