Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujenga ushirikiano kupitia vyama na mashirikisho yao ili kuhakikisha kunakuwa na mfumo rasmi na unaoeleweka wa uendeshaji wa tasnia ya sanaa nchini.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego wakati akiliahirisha Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ambapo alisema kwamba,wasanii wamekuwa walalamishi tu pasipokuchukua hatua na kuleta mabadiliko ndani ya tasnia.
“Wasanii turudi nyuma katika vyama vyetu, tujiulize kama vyama vyetu viko hai na sisi tuko ndani. Tumekuwa tukilalamika sana, malalamiko mengine ni sahihi na mengine si sahihi. Wakati umefika wa kuleta mabadiliko” alisema Materego.
Aliongeza kwamba,uwepo wa wasanii wengi hapa nchini pasipokuwa na mfumo unaowaunganisha na kuwaweka pamoja hakutakuwa na maana yoyote hivyo kuna kila sababu ya wasanii wenyewe kuamka na kuujenga mfumo huo.
“Hebu hapa tujiulize ni wasanii wangapi wako katika vyama? Sasa ni kwa vipi sauti yako itasikika wakati hauko katika umoja? Ni lazima turudi nyuma na tujipange katika vyama vyetu na kuyapa nguvu mashirikisho. Tusizungumzie mfumo wakati sisi wenyewe tuko nje ya mfumo” alitoa rai Materego.
Alizidi kueleza kwamba, BASATA katika mwaka huu wa fedha imejipanga kuendesha chaguzi za mashirikisho yote ya sanaa nchini na kuwataka wasanii kujipanga katika vyama vyao na kuhakikisha vinakuwa hai kwa ajili ya kujenga mfumo utakaoleta mageuzi ya maendeleo katika tasnia hii.
Aidha,alisikitishwa na tabia ya wasanii kutokuwa katika vyama na badala yake kukaa pembeni na kutupa lawama au kukosoa mwenendo wa tasnia pasipokuzingatia kwamba wao wanapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko na kupaza sauti zao wakiwa ndani ya mfumo.
“Tuanze kujiuliza sauti zetu zinasikika katika vyama vyetu? Kama hauko katika chama wewe ndiye unayekwamisha ujenzi wa mfumo. Wakati umefika tusiwe watu wa kulalamika bali kuleta mabadiliko ya kweli tukiwa katika umoja wetu” alihitimisha Materego.
Awali katika program ya wiki hii,Viongozi wa mashirikisho ya wasanii nchini walipata fursa ya kuwasilisha uzoefu wao kuhusu bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo iliyosomwa bungeni hivi karibuni.
0 maoni:
Post a Comment