Monday, October 10, 2011

MKUTANO MKUU WA MWAKA WA TASWA DESEMBER 17 MWAKA HUU

MKUTANO Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), utafanyika Desemba 17, 2011 eneo la Dar es Salaam Zoo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kamati ya Utendaji ya TASWA iliyokutana hivi karibuni, ilifikia uamuzi wa mkutano huo ufanyike eneo hilo lililopo Kilometa 37 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwa nia ya kuwaweka pamoja kwa siku nzima waandishi wa habari za michezo na kubadilishana mawazo kuhusiana na mambo mbalimbali yaliyotokea mwaka 2011.

Nia ya TASWA ni kumaliza Mkutano Mkuu saa nane mchana na baada ya hapo, waandishi watajumuika katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam Zoo kwa nia ya kuburudika na kutumia nafasi hiyo kupongezana kwa kazi za mwaka 2011 na kupanga mikakati ya mwaka 2012.

Kamati ya Utendaji awali ilitaka mkutano huo ufanyike Desemba 31 Bagamoyo mkoani Pwani, ili kuukaribisha kwa pamoja mwaka mpya 2012, lakini wajumbe walikubaliana ifanyike Dar es Salaam Zoo Desemba 17, kwani Desemba 31 wengi huwa wanapenda kuukaribisha mwaka na familia zao.

Kutokana na hali hiyo, TASWA inawaomba wanachama wake wote wajipange kwa ajili ya mkutano huo, ambao ajenda zake zitakuwa zile za kawaida zilizopo kwenye Katiba, ambazo ni pamoja na Ripoti ya Utendaji kwa mwaka 2010/2011, Ripoti ya Fedha 2010/2011.

Pia wanachama ambao watapenda kuwa na ajenda nyingine zijadiliwe kwenye mkutano huo wawasilishe kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa TASWA ama Katibu Msaidizi wa TASWA na mwisho wa kufanya hivyo itakuwa Novemba 30 mwaka huu.

Pia TASWA inawaomba wanachama wake wote kuhakikisha wanalipia ada zao za uanachama za mwaka 2011/2012 haraka iwezekanavyo na wawasiliane na Mhazini wa TASWA, Sultani Sikilo ama Mhazini Msaidizi Mohammed Mkangara na mwisho wa kufanya hivyo ni Desemba 10 mwaka huu.

Wengi wa wanachama walilipa ada kabla ya uchaguzi uliopita, ambayo ilikuwa ya mwaka 2010/2011.

Huu utakuwa Mkutano Mkuu wa Kwanza tangu uongozi wa TASWA chini ya Uenyekiti wa Juma Pinto uingie madarakani Agosti 15 mwaka jana.

(B)     MAFUNZO
TASWA inawashukuru wote waliofanikisha mafunzo ya waandishi wa habari za michezo yaliyofanyika Oktoba 1 na 2 mwaka huu mkoani Morogoro na kushirikisha wadau 40.

Tunawashukuru TASWA Morogoro chini ya uenyekiti wa Nickson Mkilanya kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha kufanikisha mafunzo hayo.

Pia TASWA inawashukuru wadau wake mhariri mkongwe Said Salim, mdau Anna Kibira, mwanasheria Damas Ndumbaro, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera na Alfred Selengia ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kuendeleza mpira wa wavu Tanzania kwa mada zao walizotoa kwenye mafunzo hayo.

Pia tunaishukuru kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, pamoja na Kampuni ya mabasi ya Al Saedy kwa kudhamini mafunzo hayo, tunaomba ushirikiano huo uendelee.

Juhudi zinaendelea ili kuhakikisha mafunzo yaliyopangwa kufanyika mkoani Arusha Novemba mwaka huu yanatimia kama ilivyopangwa, tunaamini hakuna lisilowezekana chini ya jua.

Nawasilisha.

Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
10/10/2011.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU