Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imemmwagia sifa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodgar Tenga, kwa utendaji wake wa kazi, hali inayowafanya wafikirie kuingia mkataba mwingine wa udhamini wa ligi ya Tanzania Bara.
Mkataba wa Vodacom na TFF unafika tamati mwezi Septemba mwaka huu, tangu walipoingia kwa mara ya kwanza, mwaka 2007 na kufanikiwa kwa vitendo kuiweka nchi pazuri, katika sekta ya michezo.
Katika udhamini huo, Vodacom wametumia zaidi ya Shilingi Bilioni 1.3 kwa ligi nzima, ikiwa ni mpango wenye dira ya kuhakikisha kwamba soka linapiga hatua.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Kitengo cha Udhamini wa Vodacom Tanzania, George Rwehumbiza, alisema kwamba mkataba wao mpya watakaoingia mwaka huu, ni matunda ya uongozi bora wa Tenga na timu yake.
Alisema wanaamini udhamini wao huo, utaweza kuinua kiwango cha mpira wa miguu, inayotarajiwa kuanza Januari 21 katika viwanja mbalimbali nchini.
"Sisi kama Vodacom tutakaa na wenzetu wa TFF kuangalia jinsi tutakavyoongeza udhamini wetu wa ligi ili kukuza zaidi michezo, ingawa tunaamini hayo ni matunda ya Tenga.
"Mdhamini hawezi kudhamini mahala kama hapana utaratibu mzuri, hivyo haya ni matarajio yetu kuwa tutapiga hatua na kuiweka nchi sehemu nzuri," alisema Rwehumbiza.
Aidha Rwehumbiza alizitaka timu zote zinazotarajia kuingia kwenye ligi hiyo kucheza kwa kujituma ili wajipatie mafanikio ya kuiweka ligi yao katika ushindani wa aina yake.
Timu hizo zinazotarajiwa kumenyana kuanzia Januari ni pamoja na Simba SC, Yanga SC, Azam FC, Mtibwa Sugar, JKT Oljoro, Coastal Union ya Tanga, Villa Squad, African Lyon, JKT ruvu, Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Toto African ya Mwanza na Moro United.
0 maoni:
Post a Comment