Mechi ya marudiano ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia (Brave Gladiators) imeingiza sh. 38,220,000.
Kiasi hicho ni kutokana na watazamaji 16,334 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa juzi (Januari 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Twiga Stars kuibuka na ushindi wa mabao 5-2.
Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 1,000 (watoto), sh. 2,000 (viti vya kijani na bluu), sh. 3,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 5,000 (VIP C na B) na sh. 10,000 kwa VIP A.
Watoto waliokata tiketi kuingia uwanja ni 634, viti vya rangi ya kijani na bluu 13,238, viti vya rangi ya chungwa 1,040, VIP B na C 1,246 na VIP A watazamaji 176.
Vilevile Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru washabiki na wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha mechi hiyo kati ya Twiga Stars na Namibia.
WAMISRI KUICHEZESHA STARS FEB 29
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Misri kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 29 za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Tanzania na Msumbiji.
Waamuzi watakaochezesha mechi hiyo namba 25 itakayochezwa Februari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni Farouk Mohamed atakayekuwa mwamuzi wa kati. Wasaidizi wake ni Ayman Degaish na B.T Abo El Sadat wakati mwamuzi wa akiba ni Ghead Grisha.
Kamishna wa mechi hiyo ni Loed Mc Ian wa Afrika Kusini. Mchezo wa marudiano kwa ajili ya fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini utafanyika jijini Maputo baadaye mwaka huu.
NAHODHA TWIGA STARS KUCHEZA UTURUKI
Nahodha wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars), Sophia Mwasikili ameondoka jana alfajiri (Januari 30 mwaka huu) kwa ndege ya Turkish Airlines kwenda Uturuki kucheza mpira wa kulipwa.
Mwasikili amekwenda kujiunga na Luleburgazgucu Spor Kulubu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Wanawake nchini humo.
Beki huyo wa kati wa Twiga Stars aliyekuwa akichezea timu ya Sayari Women amejiunga na klabu yake hiyo mpya kwa mkataba wa miaka miwili.
Awali Mwasikili alitakiwa kujiunga mapema na timu hiyo lakini alilazimika kusubiri kwanza mechi ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia (Brave Gladiators) iliyochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
0 maoni:
Post a Comment