Tuesday, January 17, 2012

TWIGA STARS YASAIDIWA VINYWAJI

Timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars leo (Januari 17 mwaka huu) imekabidhiwa msaada wa maji ya kunywa na soda ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi yake ya marudiano dhidi ya Namibia itakayochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Kampuni ya SBC Tanzania inayozalisha Pepsi, Mirinda na 7up ilikabidhi msaada wa vinywaji hivyo vyenye thamani ya sh. milioni moja kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah ambaye aliishukuru kwa kuitikia mwito wa kuisaidia Twiga Stars.
 
Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Meneja Mauzo wa SBC Dar es Salaam, Ali Masoud alisema wameitikia mwito wa TFF kutaka wadau mbalimbali waisaidie timu hiyo ambayo haina mdhamini ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano inayoshiriki.
 
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Babati (BDFA), Omari Chaka alimkabidhi Kocha wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa katoni kumi za maji ya kunywa zenye thamani ya sh. 25,000.
 
Alivitaka vyama vya mpira wa miguu vya wilaya na mikoa navyo kujitokeza kuisaidia timu hiyo badala ya kuiachia TFF peke yake kwa vile Twiga Stars ni timu ya Watanzania wote.
 
Chaka alisema ameamua kutoa msaada huo kuitikia mwito wa TFF, lakini vilevile kuguswa na maandalizi hafifu ya timu hiyo na pia ushindi wa mabao 2-0 ilioupata kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Namibia kuwania tiketi ya kucheza fainali za Nane za Kombe Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
 
Naye Mkwasa akipokea msaada huo, alisema ni mkubwa katika maandalizi yao ambapo alimshukuru Chaka, na pia kuwataka Watanzania wengine hasa Serikali kuwa mstari wa mbele kuzisaidia timu za Taifa kama inavyofanyika katika nchi nyingine.
 
Kocha huyo alisema huu ndiyo wakati muafaka kwa wadau kuisaidia Twiga Stars ikiwa katika maandalizi badala ya kusubiri ushindi upatikane ndipo wajitokeze.
 
Twiga Stars itaingia kambini kesho (Januari 18 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo dhidi ya Namibia. Iwapo itafanikiwa kuitoa Namibia itacheza na mshindi kati ya Misri na Ethiopia. Katika mchezo wa kwanza jijini Cairo, Misri iliifunga Ethiopia mabao 4-2.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU