Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kupitia kitengo chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute Resolution Chamber- DRC) limeagiza klabu ya Yanga kumlipa mchezaji John Njoroge sh. 17,159,800 ikiwa ni fidia kwa kuvunja mkataba wake kinyume cha taratibu.
Uamuzi huo wa DRC chini ya Jaji Theo van Seggelen ambaye ni raia wa Uholanzi ulifanywa Desemba 7 mwaka jana jijini Zurich , Uswisi na kutumwa TFF kwa njia ya DHL, Januari 17 mwaka huu.
Njoroge ambaye ni raia wa Kenya aliwasilisha kesi yake FIFA kupinga Yanga kuvunja mkataba alioingia wa kuichezea timu yao kinyume na makubaliano. Mchezaji huyo hivi sasa anachezea timu ya Tusker ambayo ni mabingwa wa Kenya .
Yanga ina siku nne za kukata rufani kupinga uamuzi huo kuanzia tarehe iliyoupokea kama inataka kufanya hivyo. Klabu hiyo inatakiwa iwe imeshamlipa Njoroge ndani ya siku 30 tangu ilipopokea uamuzi huo. Ikishindwa kulipa ndani ya muda huo, itatozwa riba ya asilimia 5 kwa mwaka ya fedha hizo.
Ikiwa Yanga itashindwa kulipa ndani ya muda huo vilevile suala hilo litafikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA kwa hatua zaidi.
0 maoni:
Post a Comment