Friday, February 24, 2012

KOZI YA MADAKTARI WA TIBA YA MICHEZO

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa kozi ya awali ya madaktari au wataalamu wa viungo (physiotherapist) kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza itakayofanyika jijini Dar es Salaam.
 
Kozi hiyo ya siku tano itakayoanza Machi 5-9 mwaka huu itakuwa na washiriki 32 tu. Kila klabu inatakiwa kutuma mshiriki mmoja ambapo anatakiwa kuwa daktari wa timu au physiotherapist.
 
Katika sifa za kitabibu, washiriki wanatakiwa wawe Clinical Officer (Medical Assistant), Assistant Medical Officer na Medical Officer au Physiotherapist. Ada ya kushiriki ni sh. 60,000.
 
Washiriki wanatakiwa kutuma TFF wasifu wao (CV) na nakala za vyeti vyao vya kitaaluma na mwisho wa kuthibitisha kushiriki kozi hiyo ni Machi Mosi mwaka huu. Kwa madaktari wanatakiwa wawe ambao kwa sasa wanazitumia klabu husika (active).
 
Kila klabu itamgharamia mshiriki wake kwa malazi, nauli ya kuja na kurudi pamoja na posho wakati TFF itatoa vifaa vya kozi (stationeries), chai na chakula cha mchana.
 
VIINGILIO STARS VS MSUMBIJI
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Februari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 3,000.
 
Jumla viti 36,693 (rangi ya bluu na kijani) ndivyo vitakavyotumika kwa kiingilio hicho katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 wakiwa wameketi.  
 
Viingilio vingine ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 15,000 kwa VIP B wakati kwa watakaokuwa miongoni mwa watakaokaa katika viti VIP A ambavyo viko 748 tu watalazimika kulipa sh. 20,000 kwa kila mmoja.
 
Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha mafuta cha Bigbon kilichopo Msimbazi (Kariakoo), mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio, Kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.
 
MWENYEJI KITUO CHA FAINALI FDL
Mkoa unaotaka kuwa mwenyeji wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoshirikisha timu tisa bora za ligi hiyo unatakiwa kutoa sh. milioni 25 ambazo ni gharama za kuendesha fainali hizo.
 
Haki ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo iko wazi kwa mikoa yote wanachama wa TFF ingawa tayari ipo minne ambayo imeshatuma rasmi maombi ya kuandaa fainali hizo. Mikoa hiyo ni Mbeya, Mwanza, Ruvuma na Tabora.
 
Kwa mikoa ambayo itakuwa tayari kuwa mwenyeji kwa maana ya kutimiza sharti hilo la kutoa kiasi hicho cha fedha inatakiwa iwe imefanya hivyo kufikia Machi 15 mwaka huu.
 
Pia kumefanyika mabadiliko ya kuanza fainali hizo, sasa zitaanza Machi 31 mwaka huu badala ya Machi 17 ambayo ilitangazwa awali.
 
MAPATO STARS VS DR CONGO
Pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC (Leopards) lililofanyika jana (Februari 23 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 32,229,000.
 
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 11,420 waliokata tiketi kushuhudia mechi kwa kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000 na sh. 15,000.
 
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 5,916,288, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, malipo kwa kamishna wa mchezo sh. 150,000, malipo kwa waamuzi wanne sh. 480,000, ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000, Wachina sh. 2,000,000, umeme sh. 300,000 na maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000.
 
Nyingine ni asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 3,676,542, asilimia 10 ya uwanja sh. 1,838,271, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 919,136 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 11,948,763.
 

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU