Wednesday, February 22, 2012

MeTL YAPANIA KUWEKEZA ZAIDI ZAO LA MKONGE

Zao la mkonge katika moja ya mashamba ya MeTL

Utajiri wa nchi zilizoendelea duniani (G8) umefikiwa kwa kuzingatia uongozi wa nchi hizo kuwekeza kwenye viwanda, na asilimia 90 ya uwekezaji huo hutegemea uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mazao.

Ni asilimia 10 tu ya uzalishaji wa bidhaa katika viwanda hutegemea vitendea kazi ikiwemo mashine za aina zote na vyombo vya usafiri.

Kwa kutambua kuwa viwanda ndiyo chanzo cha ukuzaji uchumi wa nchi, msisitizo kwa viongozi wa ngazi za juu serikalini huelekezwa kwenye kilimo ambapo mkulima atakapozalisha mazao yawe ya chakula aweze kujikimu kwa chakula, lakini pia awe na ziada ambayo ataiuza kwa lengo la kujiongezea kipato.

Yapo mazao ya chakula na ya biashara, na mazao ya biashara hutegemewa kukuza pato la mkulima kwa asilimia kubwa kuliko ilivyo kwa wakulima wa mazao ya chakula. Pia kilimo cha mazao hayo hukuza pato la nchi kwa kuzingatia biashara za kimataifa.

Nchini Tanzania yapo mazao mengi ya biashara, na miongoni mwa hayo ni pamoja na buni, chai, korosho, tumbaku na mkonge.
Wakati baadhi ya wananchi kutokana na hali ya jiografia ya maeneo yao hulazimika kulima aina hiyo ya mazao, baadhi hulima mazao ya chakula ambayo ni mahindi, maharagwe, mchele, viazi, ndizi na mihogo.

Katika makala haya, kubwa linalobainishwa ni jinsi kilimo cha mkonge kilivyotoa ajira kubwa kwa vijana tofauti na ilivyo kwenye uwekezaji wa aina  nyingine ya mazao, lakini ukweli wa hilo hauko wazi kwa wengi.

Sifa nyingi zinazobebwa na kilimo cha zao la mkonge ni pamoja na uchumi wa nchi ambapo nusu ya mapato ya Serikali hutokana na zao hilo, lakini pia robo tatu ya ukubwa wa kilimo ni wa zao la mkonge.

Asilimia 80 ya Watanzania wameajiriwa katika kilimo, hivyo kufanikisha sera ya Kilimo Kwanza na mfano wa wazi ni Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL).
Kampuni hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya kilimo na kuinua kiwango cha uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Mwaka 1997, kampuni hiyo iliwekeza ekari 35,000 za mkonge katika mashamba kadhaa mkoani Tanga, Kilimanjaro, Pwani na Morogoro na imeweza kufanikisha biashara ya zao hili.

Kwa uwekezaji huo, zaidi ya wafanyakazi 300 wameajiriwa kwenye mashamba ya mkonge kwa ajili ya kushughulikia zao hilo, idadi ambayo ni kubwa kwa sekta binafsi katika utoaji ajira kwa Watanzania.
Miundombinu kama nyumba za wafanyakazi, kambi za wafanyakazi, matumizi ya barabara, huduma za shule na zahanati vimeanzishwa katika mashamba yote.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mkurugenzi Mkuu wa MeTL, Mohamed Dewji maarufu kama Mo, anasema kuwa vitu vingine kama magari na vifaa vya kilimo vimewekwa katika kila shamba, hivyo kampuni imewekeza sh. bilioni 50 katika kilimo hicho.

"Mkonge ni zao pekee ambalo halihitaji maji na linaloweza kuvunwa wakati wowote. Halina mipaka ya ukame... hili ndilo la kulipa kipaumbele kwani litawainua wakulima," anasema Dewji ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini (CCM).

"Shughuli za maendeleo ya kilimo zimetoa ajira kwa zaidi ya watu 5,000 wakati wa msimu wa kilimo na tumetoa mbinu za kilimo kupitia kwa wataalamu wetu hivyo kuboresha ufahamu wa wafanyakazi wetu," anasema Mkuu wa Kitengo cha Kilimo wa MeTL, Mamik.

Katika mikoa hiyo, MeTL huzalisha tani 6,000 za mkonge kila mwaka na wanazo ekari 10,000 za mashamba hayo ambapo dhamira kuu ni kulima kati ya tani 10,00 na 15,000 ili kufanikisha kupatikana soko la nje pia.
 

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU