Saturday, February 4, 2012

RAMBIRAMBI MSIBA WA GRATIAN MATOVU

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa kimataifa Gratian Matovu kilichotokea jana saa 6 mchana (Februari 3 mwaka huu) nyumbani kwake Mbezi Beach Makonde, Dar es Salaam.
 
Licha ya kuwa mwamuzi, Matovu aliyezaliwa Novemba Mosi 1926 aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), sasa TFF mwishoni mwa miaka ya 90. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF.
 
Vilevile aliwahi kuwa mkufunzi wa waamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na pia kamishna wa shirikisho hilo.
 
Msiba uko nyumbani kwake Mbezi Beach Makonde na shughuli za kumuaga marehemu zitafanyika hapo hapo siku ya Jumatatu (Februari 6 mwaka huu) kuanzia saa 5 asubuhi.
 
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Steven Matovu baadaye mwili utasafirishwa kwenda Karagwe mkoani Kagera kwa maziko ambayo yanatarajiwa kufanyika Februari 9 mwaka huu.
 
Msiba huo ni pigo kwa familia ya Matovu, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa wakati akiwa mwamuzi na mkufunzi wa waamuzi.
 
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Matovu, Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
 
Mungu aiweke roho ya marehemu Gratian Matovu mahali pema peponi. Amina


0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU