Tuesday, February 14, 2012

TAARIFA KWA UMMA

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU MPANGO WA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA SERIKALI KWA UWAZI (OPEN GOVRNMENT PARTNERSHIP-OGP)
Tanzania imeridhia kujiunga na Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership - OGP). Mpango huu ni juhudi za kimataifa katika kuhimiza uendeshaji wa Serikali kwa uwazi zaidi, ushirikishwaji mkubwa wa wananchi, kudhibiti rushwa katika jamii na kuimarisha utoaji wa huduma bora. 

Mpango huu ulizinduliwa rasmi na Viongozi wa Nchi za Marekani, Mexico, Norway, Afrika ya Kusini, Indonesia na Uingereza tarehe 20 Septemba, 2011 wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani. Kwa kutambua umuhimu wa Mpango huu, Tanzania imeridhia kujiunga nao. Hadi sasa nchi nyingine 37 zimeridhia kujiunga zikiwemo nchi nne (4) kutoka Bara la Afrika ambazo ni Afrika ya Kusini, Ghana, Kenya na Liberia.

Vigezo vya nchi kuwa mwanachama wa Mpango huu  ni pamoja na kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa (Country Action Plan) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi na wananchi. Mambo muhimu yanayosisitizwa ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika Serikali, kuwawezesha wananchi kupata taarifa kutoka Serikalini kwa urahisi zaidi, kuzuia na kupambana na rushwa na kusisitiza matumizi ya teknolojia na uvumbuzi katika uimarishaji wa utawala bora. 

Serikali imeanza mchakato wa kutayarisha Mpango Kazi wa Kitaifa. Katika kuandaa mpango huo wananchi watashirikishwa kikamilifu ili kutoa maoni yao kuhusu maeneo yatakayozingatiwa kwenye Mpango. Njia mbalimbali za mawasiliano zitatumika kukusanya maoni ya Wananchi. Njia hizo ni pamoja na tovuti ya wananchi (www.wananchi.go.tz), barua za kawaida kupitia posta  (Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu, S.L.P. 9120, Dar es Salaam), ujumbe bila malipo kupitia simu ya mkononi (SMS) namba 0658-999222, barua pepe: ogp@ikulu.go.tz na mikutano ya majadiliano na wadau mbalimbali. 

Mkutano wa kwanza wa kukusanya maoni ya wadau ulifanyika tarehe 15 Novemba, 2011 na uliwashirikisha wawakilishi kutoka Taasisi za Kiraia, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kidini, Vyombo vya Habari na Serikali. 

Kwa kuanzia, uandaaji na utekelezaji wa Mpango huo utahusisha vipaumbele  vya sekta tatu za Afya, Elimu na Maji ili  kuimarisha uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika utoaji wa huduma. Mpango utaendelea kuongeza wigo wa utekelezaji kwa kujumuisha sekta zote kadri uzoefu utakavyopatikana.

Serikali iko tayari na imedhamiria kutekeleza Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa uwazi na inaamini kuwa Mpango huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi. Hivyo, Serikali inatoa wito na kuwakaribisha wananchi wote kutoa maoni yatakayosaidia kuandaa mpango wa kitaifa utakaosaidia kuongeza uwajibikaji, uwazi na uadilifu  katika utendaji wa kazi kwenye sekta za Afya, Elimu na Maji. Muda wa kutoa maoni ni kuanzia sasa hadi tarehe 25 Machi, 2012. Tunawaomba Wananchi, washiriki kikamilifu katika maandalizi ya Mpango Kazi wa Kitaifa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

IMETOLEWA NA OFISI YA RAIS
IKULU- DAR ES SALAAM.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU