Timu za Moro United na Villa Squad ambazo ziko kwenye vita ya kukwepa kushuka daraja katika Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinapambana kesho (Machi 28 mwaka huu) kwenye moja kati ya mechi mbili za siku hiyo.
Mechi hiyo namba 153 itachezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili. Moro United iko nafasi ya 11 ikiwa na pointi 18 wakati Villa Squad iko nafasi ya 14 kwa pointi zake 14.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 kwa jukwaa kuu. Mwamuzi atakuwa Andrew Shamba akisaidiwa na Samson Kobe na Idd Mikongoti wote wa Dar es Salaam.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Arthur Mambeta wa Dar es Salaam wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Emmanuel Chaula kutoka mkoani Rukwa.
Mechi nyingine ya Machi 28 mwaka huu itakayochezeshwa na mwamuzi Judith Gamba wa Arusha itakuwa kati ya Ruvu Shooting itakayoikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
Gamba katika mechi hiyo namba 150 atasaidiwa na Saada Tibabimale kutoka Mwanza na Hellen Mduma wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa akiba ni Juma Safisha wa Pwani wakati Kamishna ni Hamis Kissiwa wa Dar es Salaam.
Mechi za Machi 31 mwaka huu ni Coastal Union dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi ya African Lyon na Simba.
0 maoni:
Post a Comment