Friday, April 13, 2012

ULIMWENGU ATUA NGORONGORO HEROES

Mshambuliaji Thomas Ulimwengu ambaye ndiye mchezaji pekee kutoka nje aliyeitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye U20 (Ngorongoro Heroes) anatarajia kujiunga na kikosi hicho ambacho kiko kambini kesho (Aprili 14 mwaka huu).

Ulimwengu ambaye anachezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) atawasili saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways akitokea jijini Lubumbashi.

Ngorongoro Heroes ambayo iliingia kambini Aprili 20 mwaka huu inajiandaa kwa mechi ya mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Sudan. Mechi hiyo itachezwa Aprili 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Kwa mujibu wa Kocha Poulsen, kikosi chake kesho (Aprili 14 mwaka huu) kitakuwa na awamu (sessions) mbili za mazoezi kwenye Uwanja wa Karume. Awali ya kwanza itakuwa asubuhi nay a pili itafanyika jioni.

Wachezaji wengine walioko kwenye kikosi hicho cha Ngorongoro Heroes ni Saleh Malande, Aishi Manula, Hassan Kessy, Said Ruhava, Carlos Kilenge, Dizzana Issa, Amani Kyata, Issa Rashid, Emily Mgeta na Khamis Mroki.

Wengine ni Ramadhan Singano, Frank Sekule, Frank Domayo, Omega Seme, Abdallah Hussein, Ibrahim Rajab, Hassan Dilunga, Alhaje Zege, Jerome Lambele, Atupele Green na Simon Msuvan.
Mechi ya marudiano dhidi ya Sudan itachezwa jijini Khartoum kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.

Fainali za Afrika kwa vijana zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria. Timu nne za juu kwenye fainali hizo zitacheza Fainali za Dunia zitakazofanyika nchini Uturuki kuanzia Juni hadi Julai mwakani.

LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA 23
Raundi ya 23 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya 23 kesho (Aprili 14 mwaka huu) kwa mechi nne. Polisi Dodoma wataikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma wakati JKT Ruvu watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar mjini Turiani.

Mechi nyingine za raundi hiyo zitakuwa kati ya Kagera Sugar na African Lyon zitakazooneshana kazi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Nayo Moro United inaikaribisha Oljoro JKT katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Raundi ya 23 itakamilika Jumapili (Aprili 15 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Yanga itakuwa mgeni wa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza. Villa Squad itapambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 18 mwaka huu kwa mechi tano. Kagera Sugar vs Yanga mjini Bukoba, Toto Africans vs African Lyon jijini Mwanza, JKT Ruvu vs Simba- Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ruvu Shooting vs Moro United mjini Mlandizi na Polisi Dodoma vs Coastal Union mjini Dodoma.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU