Kim Poulsen ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars) kuanzia Mei 11 mwaka huu kuziba nafasi ya Jan Poulsen.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema Kim amepewa mkataba wa mwaka mmoja baada ya Shirikisho kuamua kutomuongezea mkataba Jan. Mkataba wa Jan uliokuwa wa miaka miwili unamalizika Julai 30 mwaka huu.
Amesema kwa vile Taifa Stars inakabiliwa na mechi za mchujo za Kombe la Dunia raundi ya pili Kanda ya Afrika na mechi za mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN), TFF imeona ni lazima iwe na kocha mpya mapema kabla ya mkataba wa Jan kumalizika.
Kim ambaye ni raia wa Denmark amekuwa nchini kwa mwaka mmoja sasa akifundisha timu za Taifa za vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) na miaka 20 (Ngorongoro Heroes), hivyo anawafahamu vizuri wa wachezaji wa Tanzania.
TFF imeanza mchakato wa kutafuta kocha mwingine wa timu za vijana atakayeziba nafasi ya Kim. Ili kuwa na makocha wenye falsafa moja, kocha huyo anatafutwa kutoka Denmark.
Naye Kim ambaye Jumatatu (Mei 14 mwaka huu) atatangaza kikosi cha Taifa Stars ambacho Juni 2 mwaka huu kuivaa Ivory Coast katika mechi ya mashindano amesema yuko tayari kwa kazi hiyo na kusisitiza kuwepo ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali ili timu hiyo iweze kufanya vizuri.
0 maoni:
Post a Comment