Thursday, June 14, 2012

KOCHA WA TOTTENHAM AONDOKA KATIKA KLABU HIYO

Harry Redknapp ameamua kuondoka Tottenham, baada ya kuwafundisha vijana wa Spurs kwa muda wa miaka minne,Redknapp alifikiriwa sana kama meneja ambaye angeliweza kuifundisha vyema timu ya taifa ya soka ya England, lakini hatimaye aliikosa kazi hiyo, na chama cha soka cha England kiliamua kumpa nafasi Roy Hodgson kazi hiyo.Siku ya Jumanne Redknapp alikanusha uvumi kwamba tayari alikuwa amejiuzulu kutoka Tottenham.

Redknapp, mwenye umri wa miaka 65, alikuwa amesalia na mwaka mmoja katika mkataba wake na klabu hiyo ya White Hart Lane, na inasemekana huenda ikawa kulikuwa na hali ya kutoelewana kuhusiana na mkataba mpya, baada ya kushauriana na mwenyekiti wa klabu, Daniel Levy.

Meneja huyo wa zamani wa Bournemouth, West Ham, Portsmouth na Southampton, inafahamika sasa ameachana na klabu hiyo ya mjini London.

Wakati Fabio Capello alipoiacha kazi ya meneja wa timu ya England, tarehe 8 Februari, Spurs walikuwa katika nafasi ya tatu katika ligi kuu ya Premier walikuwa wameiacha Arsenal, ambayo ilikuwa inaonekana dhaifu wakati huo, kwa pointi kumi.Hatimaye waliachwa nyuma kwa pointi nne na Arsenal, na kukosa nafasi ya kufuzu kwa mechi za klabu bingwa barani Ulaya.

Redknapp alipoondoka Portsmouth mwaka 2008, aliweza kuielekeza Tottenham hadi katika mashindano ya klabu bingwa, kwa mara ya kwanza, waliposhiriki mwaka 2010.

Baada ya kumaliza ligi kuu katika nafasi ya nne msimu uliopita, Tottenham walishindwa kufuzu, kufuatia Chelsea kupata ushindi katika fainali ya klabu bingwa.

Redknapp alifikiriwa kwanza wakati meneja kutoka Italia, Fabio Capello alipojiuzulu mwezi Februari, lakini hatimaye Hodgson ndiye aliyechaguliwa.

Alikiri kwamba ingelibidi ajiuzulu kama meneja wa Tottenham, iwapo angelipata kazi hiyo ya timu ya taifa.

Inasemekana Levy hakufurahishwa na namna Spurs walivyokamilisha msimu, na kupoteza nafasi nzuri, baada ya kuitangulia Arsenal kwa pointi kumi, na ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu.

Redknapp mara kwa mara alikanusha hali hiyo ya kudorora kwa timu yake ni kutokana na kuhusishwa na kibarua cha timu ya taifa.

Wiki iliyopita, aliitaka Spurs kupata suluhu juu ya hatma yake, na kusisitiza kwamba hali ya kutojua kitakachotokea ni jambo ambalo lingeliweza kuwaathiri wachezaji wa Tottenham.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU