CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) kimewafukuza Yanga katika mashindano ya Urafiki, kwa kitendo cha kupeleka kikosi cha vijana (Yanga B) badala ya kikosi cha wakubwa kwenye michuano hiyo kama walivyokubaliana.
Msemaji wa chama cha soka kisiwani Zanzibar Mniri Zakaria amesema, kwamba ZFA na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa
ujumla wamekerwa na kitendo kilichofanywa na uongozi wa Yanga na wamekichukulia kama ni dharau, kupeleka timu B badala ya timu A.
“Mashindano haya kuendesha ni gharama, jana Yanga wamecheza, watu wamekuja wanaona timu B, wametukana sana, wamesema ni utapeli, dhahiri mechi ijayo watu hawatakuja uwanjani. Sasa tutawahudhumia Yanga kwa gharama kubwa, wakati watu hawaendi uwanjani kuwaona watoto wao wa B. Kwa sababu hiyo, ZFA baada ya kushauriana pia na baadhi ya viongozi
wa serikali (ya Mapinduzi), tumeamua kuwarudisha watoto wa Yanga Dar es Salaam, wameondoka na boti ya saa 10:00 na watafika Dar es Salaam saa 12, kawapokeeni,”kilisema
chanzo chetu kutoka ZFA.
Chanzo hicho kilisema mashindano hayo, yalikuwa yana lengo zuri tu la kuzipa matayarisho timu zote zinazocheza michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, inayoanza Julai 14, Dar es Salaam- ambazo ni Mafunzo kwa upande wa Zanzibar na Simba, Azam na Yanga kwa upande wa Bara.
“Lakini ajabu Simba na Azam wameleta timu zao za kwanza, ila wao Yanga wanaleta watoto, sasa hii ni dharau kwetu kama ZFA na kinyume cha makubaliano yetu na wao. Ni dharau kwa falimia yote ya wapenda soka wa Zanzibar, ni dharau kwa wapenzi wa Yanga wa huku,”kilisema hicho.
Yanga pamoja na kupeleka timu B, lakini jana kilicheza soka ya uhakika dhidi ya mabingwa wa zamani wa Tanzania, Jamhuri ya Pemba na kufungwa kwa taabu mabao 3-2.
0 maoni:
Post a Comment