Didier Kavumbangu
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi , Didier Kavumbangu ametambulishwa rasmi leo katika klabu yake ya Yanga, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kukabidhiwa jezi namba 21.
Akimtambulisha mchezaji huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kwamba mchezaji huyo kutoka Atletico Olympique ya Burundi , amesaini mkataba wa miaka miwili.
Kavumbangu amefanya mazoezi leo na wenzake Uwanja wa Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza baada ya kutambulishwa kwenye mkutano huo, Didier alisema anashukuru kutua Yanga, kwa sababu ni timu ambayo amekuwa akiisikia muda mrefu tangu akiwa mdogo na atajitahidi kufanya vizuri, kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo.
“Nimefurahi kuja Yanga, nimefurahia mapokezi mazuri, na mimi naahidi nitafanya vizuri kuwafurahisha mashabiki,”alisema Kavumbangu.
Katika kikao hicho pia, mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi alikanusha uvumi kwamba amesaini Simba. “Nina mkataba wa miaka miwili na Yanga, hizo habari ni uzushi, mimi mchezaji wa Yanga,”alisema.
Yanga, ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, walianza maandalizi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana na Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mbelgiji Tom Saintefiet aliwataja wachezaji ambao hawajaanza mazoezi ni Hamisi Kiiza, ambaye ameitwa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, Ibrahim Job na David Luhende ambao bado wapo kwao Mwanza, wakati Juma Abdul bado ni majeruhi.
Tom alisema wachezaji wengine waliokosekana mazoezini jana ni wale ambao wapo timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, Frank Damayo, Omega Seme na Simon Msuva.
0 maoni:
Post a Comment