Thursday, August 2, 2012

MRISHO NGASA AKATA RUFAA

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Mrisho Khalfan Ngassa amepiga hodi Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kupinga kuuzwa kwake katika klabu hiyo, akitokea Azam FC bila kuhusishwa. 

AkizungumzA leo, Ngassa amesema kwamba hajafanya mazungumzo na Simba SC wala Azam FC juu ya uhamisho. “Mimi sijui chochote, na sikatai kuhamishwa, kwa sababu mimi soka ni kazi yangu na ninaweza kucheza popote, ila taratibu zifuatwe tu,”alisema. 


Ngassa amesema baada ya kuona mambo yanakwenda kinyume cha utaratibu, ameamua kulifikisha suala lake Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ili haki itendeke.
Mapema jana, Azam ilimuuza kwa Sh. Milioni 25 kwa klabu ya Simba na sasa Mrisho anafuata nyayo za baba yake Khalfan Ngassa, ambaye aliichezea Simba SC 1991/1992. 


Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 


Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo. 


Ngassa alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka miwili iliyoipita kwa dau la Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na kwa Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa kwa Wekundu wa Msimbazi. 


Mapema jana mchana, Stewart Hall, kocha Muingereza wa Azam FC jana alifukuzwa katika klabu hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame. 


Habari ambazo Blog hii  ilizipata kutoka ndani ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa anafundisha timu ya vijana. 


Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi. 


Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena. 


Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0. 


Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mbali na Ngassa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ naye pia alikkuwa katika wakati mgumu na juzi inadaiwa alionekana akilia wakati anazungumza na kiongozi mmoja wa Azam, akiuliza ni lipi kosa lake. Hata hivyo, vyanzo vinasema Sure na Azam wamemalizana salama na wataendelea kuwa pamoja. 


Sure Boy, ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya vijana ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ juzi na jana hakufanya mazoezi, lakini leo ameanza. 


Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine. Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU