Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya nne kesho (Septemba 28 mwaka
huu) kwa mechi za Super Weekend ambazo zitaoneshwa moja kwa moja (live)
na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
Mechi
ya kwanza ambayo itachezwa kesho itakuwa kati ya Azam na JKT Ruvu
Stars. Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itaanza
saa 1 kamili usiku kwa viingilio vya sh. 3,000 mzunguko, sh. 5,000 kwa
VIP C na VIP B wakati VIP A kiingilio kitakuwa sh. 10,000.
Jumamosi
(Septemba 29 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Simba na Tanzania
Prisons itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11
kamili jioni. Yanga na African Lyon zitapambana Jumapili (Septemba 30
mwaka huu kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 11 kamili jioni.
Uwanja
wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam wenyewe utakuwa mwenyeji
wa mechi kati ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar itakayochezwa Oktoba 1
mwaka huu kuanza saa 10.30 jioni. Mechi ya mwisho ya Super Weekend
itachezwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
ikizikutanisha Yanga na Simba kuanzia saa 1 kamili usiku.
RAMBIRAMBI MSIBA WA ERASTO ZAMBI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha Katibu Mkuu mstaafu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC),
Erasto Zambi kilichotokea jana (Septemba 26 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam kutokana na maradhi.
Zambi
ambaye anatarajiwa kuzikwa Jumapili (Septemba 30 mwaka huu) kabla ya
kuwa kiongozi TOC, kwa muda mrefu alikuwa mwalimu wa michezo katik Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo wanamichezo wengi hasa waliokuwa
wanafunzi katika chuo hicho wamepita kwake.
Msiba
huo ambao uko nyumbani kwake Ubungo Kibangu, Dar es Salaam ni pigo kwa
familia ya Zambi, TFF na wanamichezo kwa ujumla nchini kutokana na
mchango na mawazo aliyotoa kwa shirikisho wakati akiwa kiongozi wa TOC.
TFF
inatoa pole kwa familia ya Zambi, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na
uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya
marehemu Zambi mahali pema peponi. Amina
0 maoni:
Post a Comment