KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA), iliyokutana katikati ya wiki jijini Dar es
Salaam imekubaliana na mapendekezo ya baadhi ya wanachama kuomba isogeze mbele
kwa wiki moja Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika Desemba 21
na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani Pwani, hivyo sasa
utafanyika Desemba 28 na 29 mahali hapo hapo.
Hatua hiyo ya kusogeza
mbele inatokana na baadhi ya wanachama kuomba iwe hivyo kutokana na Jumamosi ya
Desemba 22 kutakuwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu ya soka ya
Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ile ya Zambia ‘Chipolopolo’ kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Kwa msingi huo tumekubaliana
na hoja kwamba mchezo huo kwa kiasi fulani ungeathiri umakini wa wajumbe kwenye
mkutano kwa namna moja au nyingine, hivyo kupunguza tija.
Tunaamini idadi kubwa ya
wanachama waliothibitisha kushiriki ni ishara kwamba wengi wanataka kujumuika
kwa asilimia kubwa katika kukijenga chama chao, hivyo hatuoni sababu ya kufanya
mkutano kwa kukurupuka.
Hadi kufikia Desemba 15
ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya wanachama kuthibitisha ushiriki wa mkutano
zaidi ya asilimia 95 ya wanachama walikuwa wamethibitisha kushiriki.
Kutokana na hali hiyo wote
waliothibitisha ushiriki huo na ni hai watajulishwa kwa barua rasmi, ambazo
zitaeleza utaratibu wa namna ya kufika Bagamoyo na mambo mengine muhimu
yatakavyokuwa.Barua zitaanza kutoka wakati wowote kuanzia Jumatano ijayo baada
ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kinachotarajiwa kufanyika siku hiyo.
Pia tayari TASWA
imewaalika wadau mbalimbali wakiwemo wahariri wakongwe ambao wamethibitisha
kushiriki kwenye mkutano huo wa aina yake.TASWA baada ya kupata udhamini wa Zantel
kwa ajili ya mkutano huo bado inaendelea
na mazungumzo na wadhamini mbalimbali na inatarajia kuwatangaza wakati wowote
mambo yatakavyokuwa mazuri.
(B)
Pongezi
TASWA inawapongeza
viongozi wapya wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) walioingia madarakani
Desemba 8, mwaka huu mkoani Dodoma, ambapo Ghullam Rashid alichaguliwa tena
kuwa Rais, huku Filbert Bayi akichaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu.
Tunaahidi kuendelea
kushirikiana na uongozi wa TOC kama ilivyokuwa wakati uliopita na kuwatakia
kila la kheri katika kutekeleza majukumu yao na tuna imani watafanya vyema.
(C)
Msiba:
Tumepokea kwa masikitiko
makubwa taarifa ya msiba wa mwandishi wa zamani wa habari za michezo, Amina
Singo kilichotokea usiku wa kuamkia leo.
Tunaungana na familia ya
marehemu katika kipindi hiki kigumu kwani wakati wa uhai wake alikuwa mdau
mkubwa wa TASWA wakati huo akiwa mtangazaji wa habari za michezo wa Redio Times
FM, hivyo kifo chake ni pengo kubwa kwa tasnia ya uandishi wa habari hapa
nchini.
Kwa mujibu wa marafiki za
marehemu msiba upo Mbezi na mipango ya mazishi inaendelea. Tukipata taarifa
zaidi tutajulishana.
0 maoni:
Post a Comment