Friday, March 8, 2013

KAIJAGE KOCHA MPYA TWIGA STARS

 
ROGASIAN Kaijage ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake, Twiga Stars baada ya kocha wa zamani, Charles Boniface Mkwasa kujiuzulu katikati ya mwaka jana.

Mkwasa, ambaye alikuwa nyota wa Yanga na Taifa Stars, alijiengua kufundisha timu hiyo aliyoiongoza kwa muda mrefu, baada ya Twiga Stars kuondolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika nchini Equatorial Guinea.

Twiga ilipata bao muhimu la ugenini jijini Addis Ababa ilipofungwa na wenyeji wao Ethiopia mabao 2-1, lakini ikiwa na matumaini ya kutumia vyema bao la ugenini ilijikuta ikilala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo wa marudiano na hivyo kukosa tiketi ya kurudi tena kwenye fainali hizo.

Kaijage ambaye kwa sasa anajihusisha na mradi wa vijana (grassroots) pamoja na programu nyingine za kukuza vipaji zilizo chini ya TFF, aliteuliwa na Kamati ya Ufundi ya TFF kufanya kazi hiyo na ameita kikosi cha Twiga Stars kwa mazoezi ya siku kumi kuanzia Machi 10 hadi 23 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Wachezaji walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden), Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar), Esther Chabruma (Sayari), Esther Mayalla (TSC Academy), Etoe Mlenzi (JKT), Evelyn Sekikubo (Mbarahati Queens), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma Mustafa (Sayari) na Fatuma Omari (Sayari).

Flora Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Maduka (Bujora), Hellen Peter (JKT), Irene Ndibalema (TSC Academy), Maimuna Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens), Mwanahamis Omari (Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa (Sayari).

Nabila Ahmed (Marsh Academy), Nasiria Hashim (Zanzibar), Pulkeria Charaji (Sayari), Rukia Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Luleburgaz Gucu Spor, Uturuki), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati Queens).

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU