Thursday, April 18, 2013

MECHI YA MGAMBO, YANGA YAINGIZA MIL 24/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Mgambo Shooting na Yanga iliyochezwa jana (Aprili 17 mwaka huu) Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga imeingiza sh. 24,865,000 kutokana na watazamaji 4,386.


Viingilio katika mechi hiyo namba 162 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 vilikuwa sh. 10,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 5,547,337.50 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 3,792,966.10.


Asilimia 15 ya uwanja sh. 2,820,680.08, msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 90,000, waamuzi sh. 270,000, maandalizi ya uwanja sh. 100,000 na tiketi sh. 1,587,500.


Mgawo mwingine ni gharama za mechi sh. 1,692,408.05, Kamati ya Ligi sh. 1,692,408.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 846,204.05 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) sh. 658,158.69.


MAKOCHA AZAM, FAR RABAT KUTETA.

Makocha wa timu za Azam, Stewart John Hall na AS FAR Rabat ya Morocco, Abderazzak Khairi watakutana na waandishi wa habari kesho (Aprili 19 mwaka huu) kuzungumzia mechi yao itakayofanyika Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Mkutano huo ambao pia utawahusisha manahodha wa timu hizo mbili utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Barabara ya Uhuru na Shaurimoyo.


Timu hizo zitakutana katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi ya marudiano itachezwa nchini Morocco wiki mbili baadaye.


JKT RUVU, YANGA KUUMANA JUMAPILI.

Yanga ambayo inafukuzia kwa karibu taji la Ligi Kuu ya Vodacom itapambana na JKT Ruvu katika mechi pekee ya ligi hiyo wikiendi hii itakayofanyika Jumapili (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Mbali ya mechi hiyo, nyingine zitakazochezwa mwezi huu ni kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayofanyika Aprili 24 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati Aprili 25 ni kati ya Ruvu Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Nayo Coastal Union itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mechi itakayochezwa Aprili 27. Uwanja wa Taifa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Simba na Polisi Morogoro itakayofanyika Aprili 28.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU