Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwatangazia wadau wa mpira
wa miguu kuwa ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
utawasili nchini Jumatatu (Aprili 15 mwaka huu) kwa ajili ya
kushughulikia mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka FIFA, ujumbe huo utaongozwa na Mkuu wa Idara
ya Uanachama ya FIFA, Primo Covarro na utafanya kazi kwa siku tatu
kuanzia siku ya ujio na kuondoka Aprili 18 mwaka huu.
Ukiwa
nchini, ujumbe huo utakutana na wagombea uongozi walioathiriwa na
uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambao waliomba mashauri
yao yaangaliwe upya, wagombea ambao walikata rufani FIFA, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Rufani na Sekretarieti ya TFF.
Wajumbe
hao wangependa kukutana na waziri anayehusika na michezo, hivyo TFF
imeiandikia Wizara ikipendekeza kuwa ujumbe huo ukutane na Waziri na
wakuu wengine wa michezo Aprili 16 mwaka huu 2013 kabla ya kuanza kazi
zao.
Wagombea watakaosikilizwa na ujumbe huo wa FIFA ni:
1. Farid
Salim Mbaraka Nahdi: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji
ambaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi na baadaye rufani yake kwa
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kutupwa na hali kadhalika ombi lake
la kutaka shauri lake liangaliwe upya, kukataliwa.
2. Elliud
Peter Mvella: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye
alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kukata rufani Kamati ya Rufani
ya Uchaguzi ya TFF kabla ya maombi yake ya kutaka shauri lake kuangaliwa
upya, kukataliwa.
3. Mbasha
Matutu: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye
alikatwa na Kamati ya Uchaguzi na kukata rufani ambayo pia ilitupwa
kabla ya kuomba shauri lake liangaliwe upya, ombi ambalo lilikataliwa.
4. Hamad
Yahya: Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye
alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata
rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na
kuondolewa. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini Kamati ya Rufani
ya Uchaguzi ya TFF ikatupa ombi lake.
5. Jamal
Emily Malinzi: Mgombea wa nafasi ya urais wa TFF ambaye alipitishwa na
Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo
ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, hivyo kuondolewa
kwenye mchakato. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini
likakataliwa. Hata hivyo, alikuwa ameshakata rufani FIFA.
6. Michael
Wambura: Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ambaye alikatwa na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF na rufani yake kukataliwa na Kamati ya Rufani
ya Uchaguzi ya TFF. Hakuomba shauri lake liangaliwe upya, lakini alikata
rufani FIFA.
Shirikisho
linawaomba wote waliotajwa hapo juu kujiandaa kwa utetezi na maelezo ya
kutosha na kwamba barua za kuwaita zinafuata. (Orodha ya waathiriwa na programu ya ujumbe wa FIFA imeambatanishwa)
YANGA, OLJORO KUUMANA MECHI ZA VPL
Ligi
Kuu ya Vodacom inaendelea kesho (Aprili 13 mwaka huu) kwa mechi mbili
zitakazochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sokoine jijini Mbeya.
Yanga
itakuwa mwenyeji wa Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa
Sokoine utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Tanzania Prisons na Ruvu
Shooting.
Ligi
hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili 14 mwaka huu) kwa mechi kati ya
wenyeji Azam na Simba. Mechi hiyo namba 155 itachezwa kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
WASHELISHELI KUICHEZESHA AZAM CAF
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Shelisheli
kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati
ya Azam na AS FAR ya Morocco itakayofanyika Aprili 20 mwaka huu Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi
hao ni Emile Fred atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Steve Maire na
Jean Ernesta. Mwamuzi wa mezani (fourth official) atakuwa Jean Claude
Labrossa. Kamishna wa mechi hiyo ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda.
Wakati
huo huo, CAF imemteua Mtanzania Alfred Lwiza kuwa Kamishna wa mechi ya
kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Liga Muculmana
ya Msumbiji na Wydad Casablanca ya Morocco.
Mechi
hiyo itakayochezwa kati ya Aprili 19,20 au 21 mwaka huu nchini Msumbiji
itachezeshwa na waamuzi kutoka Zimbabwe wakiongozwa na Ruzive Ruzive.
0 maoni:
Post a Comment