Thursday, April 4, 2013

WADAU WA MICHEZO WATAKIWA KUACHA KULALAMA

 Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo . Leonard Thadeo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akizungumza na washiriki

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi na viongozi wa michezo.
 
WADAU wa Michezo wameshauriwa kuacha tabia ya kulalamika mara kwa mara pale wanaposhindwa katika mashindano ya michezo mbalimbali badala yake watumie mafunzo walioyapata ili kuendeleza sekta ya michezo Tanzania.

Ushauri huo ulitolewa jana jioni na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Bw. Leonard Thadeo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Fenella Mukangara wakati wa kufunga mafunzo ya michezo ya siku mbili yaliyoshirikisha wadau hao kutoka mikoa  mbalimbali yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Alisema wamekuwa wakipata mafunzo hayo mara kwa mara, hivyo changamoto iliyoko kwao  ni kwamba wanayatumiaje katika kuboresha sekta hiyo ili kuiwezesha Tanzania kushiriki na kushinda michezo ndani na nje ya nchi.

Aidha Bw. Thadeo amewataka wadau hao  kuwa wabunifu na kujitahidi kutimiza wajibu wao kwa kutumia fursa waliyoipata kusaidiana na wanamichezo wengine waliowaacha  mikoani ili kuweza kuboresha michezo kwa sababu wote goli lao ni moja la kutaka kuinua michezo Tanzania na kuweza kupata ushindi.

Aliwataka wadau hao kuwa wabunifu ili kubuni mbinu mbadala za kuinua sekta ya michezo Tanzania na kusaidiana na wanamichezo wengine waliopo mikoani.

Aliongeza kuwa   mafunzo hayo yatakuwa ni endelevu. Pia serikali ina mpango wa kuanzisha  shahada ya pili ya michezo kwa njia ya mtandao ili kuinua michezo kuanzia ngazi ya chini hadi za juu.

Naye Mratibu wa mafunzo hayo Dk. Imani Silver Kyaruzi, aliwapongeza wadau  hao kwa kuonyesha jitihada, kuchangia na kutaka kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya michezo.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU