Mkuu wa Kitengo cha kuzuia Madawa ya Kulevya Mkoa wa Arusha Mrakibu
Msaidizi wa Polisi (ASP) Abeny Mgode akiwaonyesha waandishi wa habari
madawa ya kulevya aina ya bangi baada ya jeshi hilo mkoani hapa kukamata
magunia sita ya madawa hayo.
Gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T. 526 BWX
lililokamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa arusha likionekana kutolewa
viti vya nyuma hivyo kuweza kubeba magunia sita ya madawa ya kulevya
aina ya bangi kwa urahisi.
Mapambano dhidi ya uzuiaji wa madawa ya kulevya mkoani Arusha
yanazidi “kupamba moto” baada ya jeshi la Polisi Mkoani hapa kukamata gari
lililokuwa na magunia sita ya bangi. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa mwezi wa
April muda wa saa 6:00 Mchana wilayani Longido.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi
wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilifanikiwa baada ya askari
wa jeshi hilo kupata taarifa toka kwa raia wema juu ya kuwepo kwa tukio la
kusafirisha madawa hayo toka Longido Mjini kuelekea Namanga.
Alisema askari walipopata taarifa hiyo walianza kulifualia
gari hilo aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T. 526 BWX na mara baada
ya dereva wa gari hilo kugundua anafuatiliwa aliamua kulitelekeza na kisha
kukimbia.
“Mara baada ya askari kulifikia gari hilo walilipekua na
kukuta gunia sita za madawa ya kulevya aina ya bangi zikiwa nyuma ya siti na
mpaka hivi sasa mmiliki wa gari hilo bado hajajulikana na tunafanya juhudi za
kumtafuta”. Alisema Kamanda Sabas.
Aidha kwa upande mwingine Kamanda Sabas aliendelea
kuwashukuru baadhi ya wananchi wa Mkoa huu kutokana na ushirikiano mzuri juu ya
utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa jeshi hilo hali ambayo inasaidia
kuzuia vitendo vya uhalifu na kukamatwa kwa wahalifu wa matukio mbalimbali.
Aliendelea kuwasihi
wakazi wa mkoa huu na mikoa mingine hapa nchini kuendelea kushirikiana na jeshi
hilo katika kupeana taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuweza kuzidi kuimarisha
hali ya amani na utulivu.
0 maoni:
Post a Comment