Upangaji
ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) umefanyika leo (Mei 7
mwaka huu) huku mabingwa wa mikoa ya Dar es Salaam (Red Coast), Lindi
(Kariakoo) na Kigoma (Saigoni) wakianzia nyumbani katika ligi hiyo
itakayoanza Mei 11 au 12 mwaka huu.
Ligi
hiyo itachezwa kwa mtoano kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ambapo
mwenyeji atapanga tarehe ya mechi ambazo zinatakiwa kuchezwa kati ya
Jumamosi au Jumapili. Mechi za marudiano katika raundi hiyo ya kwanza
zitachezwa kati ya Mei 18 na 19 mwaka huu.
Katika
upangaji huo ulioshuhudiwa na waandishi wa habari kwa niaba ya klabu
husika, mabingwa wa Mkoa wa Shinyanga (Stand Ngaya FC) wamepita moja kwa
moja hadi raundi ya pili itakayochezwa kati ya Mei 25 na 25 mwaka huu
wakati mechi za marudiano ni kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.
Raundi
ya tatu itachezwa kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati marudiano ni
Juni 15 au 16 mwaka huu. Raundi ya nne itachezwa kati ya Juni 22 au 23
mwaka huu wakati marudiano ni Juni 29 au 30 mwaka huu. Raundi ya tano ni
kati ya Julai 6 na 7 mwaka huu na marudiano ni Julai 13 au 14 mwaka
huu.
Timu
tatu ndizo zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu
ujao, ambazo ni ya kwanza nay a pili wakati timu ya tatu itapatikana kwa
timu zilizoshindwa hatua ya nusu fainali kucheza zenyewe kwa zenyewe.
Washindi wa nusu fainali nao watacheza wenyewe kwa wenyewe ili kupata
bingwa wa RCL ambaye atakabidhiwa kombe la ubingwa.
Ligi
hiyo inashirikisha mabingwa kutoka mikoa 27 ya kimpira ambapo katika
raundi ya kwanza wanaanza mabingwa 26, raundi ya pili ni mabingwa 14
wakijumuisha na bingwa wa Shinyanga ambaye katika draw ameingia moja kwa
moja katika hatua hiyo.
Raundi
ya tatu itashirikisha timu saba zilizosonga mbele pamoja na moja yenye
uwiano mzuri wa matokeo ili kufanya jumla ya timu nane. Raundi ya nne
itakuwa na timu nne. Wakati raundi ya tano itakuwa ni kumpata bingwa na
mshindi wa tatu.
Katika
upangaji huo wa ratiba mechi za raundi ya kwanza (timu ya kwanza
ikianzia nyumbani) itakuwa kama ifuatavyo; Red Coast vs Abajalo,
Kariakoo vs Mtwara, Friends Rangers vs Kiluvya United, TECKFOLT FC vs African Sports, Machava FC vs Flamingo SC, Gunners United vs Manyara na Simiyu vs Magic Pressure FC.
Nyingine
ni Polisi Jamii Bunda FC vs UDC FC, Geita vs Biharamulo SC, Saigoni SC
vs Tabora, Katavi Warriors vs Rukwa United, Mji Njombe vs Mbinga United
na Kimondo FC vs Iringa.
Mechi
zitachezwa katika viwanja vya makao makuu ya mikoa, vinginevyo kuwepo
na maombi rasmi ambayo yatakubaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
SIMBA, MGAMBO SHOOTING UWANJANI KESHO
Timu
za Simba na Mgambo Shooting ya Tanga zinaumana kesho (Mei 8 mwaka huu)
katika mchezo pekee wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaofanyika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio
katika mechi hiyo itakayoanza saa 10.30 jioni vitakuwa sh. 5,000 kwa
viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000
kwa VIP C na B wakati VIP A ni sh. 20,000.
RUVU SHOOTING, SIMBA ZAINGIZA MIL 17.
Mechi
namba 111 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Simba
iliyochezwa juzi (Mei 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
na kumalizika kwa Simba kushinda mabao 3-1 imeingiza sh. 17,700,000.
Watazamaji
3,163 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa
sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata
mgawo wa sh. 3,485,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 2,700,000.
Kiingilio
cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata
tiketi hizo walikuwa 2,901 na kuingiza sh. 14,505,000 wakati idadi ndogo
ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki
28 na kuingiza sh. 560,000.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,772,416.50,
tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 1,063,449.90, Kamati ya Ligi
sh. 1,063,449.90, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
531,724.95, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
206,781.93 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh.
206,781.93.
0 maoni:
Post a Comment