Friday, June 21, 2013

LUHENDE AONGEZWA KIKOSINI TAIFA STARS

Beki wa Yanga, David Luhende ameongezwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Kocha Kim Poulsen amesema kutokana na uamuzi huo wa kumuongeza beki huyo wa kushoto amemuondoa mchezaji mmoja kwenye kikosi chake. Mchezaji huyo ni mshambuliaji Zahoro Pazi wa JKT Ruvu.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager sasa itaingia kambini kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam, Julai 3 mwaka huu badala ya Julai 4 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Mechi ya Uganda itachezwa Julai 13 mwaka huu, saa 9 kamili alasiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati ile ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye jijini Kampala, Uganda.

Wachezaji wanaotakiwa kambini ni Aggrey Morris (Azam), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruni Chanongo (Simba), John Bocco (Azam), Juma Kaseja (Simba), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar) na Kelvin Yondani (Yanga).

Wengine ni Khamis Mcha (Azam), Mrisho Ngasa (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), Mwadini Ali (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Simon Msuva (Yanga) na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).

TIMU NNE KUCHEZA NUSU FAINALI RCL.

Timu nne zimefuzu kucheza hatua ya nne (nusu fainali) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) baada ya kushinda mechi zao za hatua ya tatu ya michuano hiyo itakayotoa washindi watatu watakaocheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

Katika hatua hiyo Polisi Jamii ya Mara itaikaribisha Kimondo SC ya Mbeya kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma wakati Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Friends Rangers ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Azam Chamazi.

Mechi za kwanza zitachezwa Juni 23 mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika kwenye viwanja vya Sokoine jijini Mbeya na Kambarage mjini Shinyanga, Juni 30 mwaka huu.

Kwenye hatua ya tatu ya RCL, Friends Rangers iliing’oa Kariakoo ya Lindi kwa jumla ya mabao 2-0, Stand United FC ikaitoa Machava FC ya Kilimanjaro kwa mabao 2-1, Kimondo SC ikaishinda Njombe Mji mabao 6-5 wakati Polisi Jamii iliitambia Katavi Warriors kwa mabao 7-6.

Hatua ya mwisho ya ligi hiyo itachezwa Julai 3 mwaka huu kwa mechi za kwanza wakati zile za marudiano zitakuwa Julai 7 mwaka huu.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU