Wachezaji wa Timu ya Taifa, Taifa Stars wakiwasili katika
Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jumapili usiku baada ya kurejea
kutoka Kampala Uganda. Taifa Stars inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium
Lager.
Licha ya Taifa Stars kushindwa kufuzu kucheza katika
mashindano ya CHAN mwakani baada ya kufungwa na Uganda Cranes 3-1, wadhamini wa
Stars, Kilimanjaro Premium Lager wamesema hawajakata tama nab ado wana imani na
timu nzima na kocha Kim Poulsen.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya Stars kuwasili,
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema licha ya
habari hizi kutokuwa njema kwa watanzania, ni vizuri kukubali matokeo na
kuangalia picha kubwa na malengo ya muda mrefu.
“Ni vyema tukumbuke kuwa kwenye mpira kuna kushinda na
kushindwa,” alisema Bw Kavishe na kuongeza, “Tunapenda kuwahakikishia
watanzania kuwa sisi kama wadhamini hatujakata tama na bado tuna imani na timu
hii na kocha Kim Poulsen kwa hivyo tunawaomba watanzania wasife moyo.”
Alisema wakati walipoanza
kuidhamini Taifa Stars mwezi Mei mwaka jana na kuwekeza zaidi ya shilingi
bilioni mbili kwa mwaka, kwa muda wa miaka mitano, walikuwa na malengo kadhaa
ikiwemo kuinua hadhi ya Timu ya Taifa, kuhakikisha wanaingia kambini kwa muda
unaotakiwa, wanalipwa vizuri, wanakula na kulala vizuri na kusafiri vizuri.
“Tumejitahidi kufanya mambo haya kwani wachezaji sasa hivi
wana DVD zenye maelezo yao, tumewapa suti mpya na za kisasa na pia tumewapa
basi jipya la kisasa. Mambo haya yote pamoja na mambo wanayofundishwa na
Mwalimu Kim Poulsen yamesaidia kuleta mabadiliko kwa timu ya Taifa,” alisema.
Alisema kuna mafanikio mazuri ya timu ya taifa ambayo
watanzania lazima wayakumbuke kama kuzifunga timu kama Zambia, Cameroon, Morocco
na Kenya .
Kwa mujibu wa Meneja huyo walipoanza udhamini Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 145 kwa
mujibu wa FIFA lakini sasa imesogea hadi 109. “Haya ni mafanikio makubwa kwani
tumesogea hatua zaidi ya 40,” alisema.
Alisema safari ya mafanikio katika mpira ni ndefu na
inahitaji uvumilivu wa hali ya juu na kuongeza kuwa Kocha Kim Poulsen anafanya
kazi nzuri ya kuibua vijana.
“Kocha anahitaji kuungwa mkono na sisi sote kuanzia kwa TFF,
sisi wadhamini na watanzania wote. Tunahitaji kuangalia picha kubwa,” alisema
na kuongeza,”Nawaomba watanzania tuwe wazalendo wakati huu hii ni timu yetu na
tunatakiwa kujivunia. Vyombo vya habari pia viwe mstari wa mbele kuonesha
uzalendo.”
Alisema mechi dhidi
ya Gambia itakayochezwa mwezi wa 9 ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia ni muhimu
hata kama Tanzania haisongi mbele kwani itasaidia katika ngazi za FIFA.
0 maoni:
Post a Comment