Thursday, September 5, 2013

NYOTA WA AIRTEL RISING STARS KWENDA NIGERIA

Timu za wavulana na wasichana wenye umri chini ya miaka 17 ambazo zitaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ya Airtel Rising Stars zinaingia kambini jijini Dar es Salaam kesho (Alhamisi September 5) kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kukwea pipa kwenda nchini Nigeria kushiriki michuano hiyo. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo (Jumatano Sept 4), Ofisa Uhusiano wa Airtel Tanzania Jane Matinde alisema wachezaji hao chipukizi watashughulikia na kukamilisha hati zao za kusafiria kati ya kesho, Alhamisi na Ijumaa. “Kwa upende wetu kila kitu kimekamilika kwa ajili ya safari kuelekea kwenye mashindano hayo ya kimataifa ambayo yatashirikisha timu kutoka sehemu mbali mbali barani Afrika,” alisema.

Jumla ya wavulana na wasichana 32 walifuzu kwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu wakati wa fainali za Taifa za Airtel Rising Stars zilizofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Juni. Mashindano haya ya kimataifa yanafanyika kwa  mara ya pili mwaka huu yakiwa na lengo la kutoa fursa zaidi kwa wachezaji chipukizi kuendeleza vipaji vyao.

Kwa mara ya kwanza mashindano ya kimataifa ya Airtel Rising Stars yalifanyika jijini Nairobi mwaka jana ambapo Tanzania iliwakilishwa na timu ya wavulana pekee ambayo hata hivyo ilitolewa hatua za awali huku timu ya Nigeria ikitawazwa kuwa mabingwa.

“Kulingana na kiwango cha kuridhisha cha wachezaji waliochaguliwa mwaka huu nina imani kwamba timu zetu za Tanzania – wasichana na wavulana – wana nafasi nzuri ya kufanya vizuri,” anasema Matinde ambaye ni mmoja wa maofisa wa Airtel Tanzania waliongoza na timu kwenye mashindano hayo.

Airtel imeanzisha mashindano haya ya vijana barani Afrika kwa nia ya kusaidia upatikanaji wa vijana wenye vipaji vya soka kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ngazi ya Taifa. Airtel Rising Stars inatoa fursa kwa vijana kudhihirisha uwezo wao kwa makocha wa Taifa na kimataifa na kuweza kujiendeleza zaidi kisoka.
Hivi sasa Airtel Rising Stars ni moja ya matukio muhimu ya kisoka kwenye kalenda ya Shirikisho la Mpira wa miguu nchini (TFF). Huanzia katika hatua ya usajili ikifuatiwa na mechi za mtoano ili kupata wachezaji nyota wa kuunda timu za mikoa ambazo huchuana katika ngazi ya Taifa.

Airtel inaendesha muchuano hii kwa kushirikiana na klabu maarufu duniani ya Manchester United ambayo hutoa ushauri wa kiufundi na michuano hii imekuwa na hamasa kubwa katika nchi zote zinazoshiriki.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU