Friday, September 13, 2013

RAIS TENGA AIPONGEZA KAMATI YA LIGI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu ilipokabidhi Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) katika mzunguko wa pili msimu uliopita.

Amesema TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi kwa lengo la kutaka klabu zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo limeleta mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa marefa na makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

“Fedha za udhamini sasa zinakwenda moja kwa moja kwenye Kamati ya Ligi. Ni matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani tumeanzisha jambo hili kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Rais Tenga amesema mahali penye utulivu na utawala bora watu wanakuwa na imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni lazima kwa kampuni kuwekeza kwa vile kunakuwa hakuna vurugu.

Amesema ukiondoa Afrika Kusini na Angola katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo yenye udhamini mkubwa kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo ya televisheni.

Pia amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za Ligi Kuu hazitaruhusiwa kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti zao za mapato na matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika zijiandae kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.

Kuhusu tiketi za elektroniki, Rais Tenga amesema bado linafanyiwa kazi na CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na liko katika hatua nzuri, kwani nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza haraka iwezekanavyo.

“Tiketi za elektroniki zimechelewa kuanza kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika, lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu katika karibu viwanja vyote. Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer (mashine za kuchapia), zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa Taifa, system (mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa tunaangalia uwezekano wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa Taifa una system yake tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala lisitucheleweshe,” amesema.

WACHEZAJI 620 WATHIBITISHIWA USAJILI FDL
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imethibitisha usajili wa wachezaji 620 kati ya 624 wa timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza kutimua vumbi kesho (Septemba 14 mwaka huu).

Wachezaji wanne ambao usajili wao umezuiwa mpaka watakapokamilisha taratibu ni Emmanuel Simwanza Namwando wa African Lyon, Godfrey Bonny Namumana (Lipuli FC), na Enyinna Darlington na Chika Keneth Chukwu wote wa Mwadui FC ya Shinyanga.

Darlington na Chukwu ambao wote ni Wanigeria wamezuiwa mpaka watakapowasilisha vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji wakati Namumana aliyekuwa akicheza nchini Nepal bado hajapata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Nayo African Lyon imetakiwa kufikia muafaka na AYOSA Academy ambayo Namwando anatoka juu ya usajili kabla ya kuanza kumtumia mchezaji huyo.

Klabu ambazo zimemaliza nafasi zote 30 usajili katika FDL ni Friends Rangers FC ya Dar es Salaam, na Stand United FC ya Shinyanga wakati iliyosajili wachezaji wachache zaidi ni Burkina Faso FC. Klabu hiyo ya Morogoro imesajili wachezaji 19 tu.

Vilevile Kamati hiyo vilevile imethibitisha usajili wa wachezaji wanane wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) waliosajiliwa katika hatua ya pili ya usajili iliyoanza Agosti 14 hadi 30 mwaka huu.

Wachezaji hao ni Samir Ruhava na Amani Simba (Ashanti United), Robert Machucha na Said Ndutu (Yanga U20), Ayoub Masoud na Abdallah Selemani (Coastal Union U20), Ramadhan Kipalamoto (Simba U20) na Henry Joseph (Simba) ambaye tayari Hati yake Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imeshawasili.

SIMBA UWANJA WA TAIFA, YANGA IKO MBEYA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya tatu kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa timu zote 14 kushuka viwanjani huku masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar na ile kati ya Mbeya City na Yanga.

Simba inaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma. Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.

Pia Azam TV itautumia mchezo huo kwa ajili ya mazoezi (broadcast training) kwa wafanyakazi wake. Hivyo mechi hiyo haitarekodiwa au kuoneshwa moja kwa moja.

Katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, shughuli itakuwa kati ya mabingwa watetezi Yanga na wenyeji wao Mbeya City SC. Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna wa mechi hiyo James Mhagama kutoka Songea.

Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting na Mgambo Shooting (Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani), Oljoro JKT na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Kagera Sugar na Azam (Uwanja wa Kaitba, Bukoba), na Ashanti United na JKT Ruvu (Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam).

MJINI MAGHARIBI KUCHEZA FAINALI COPA
Mjini Magharibi imepata tiketi ya kucheza fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 upande wa wavulana baada ya kuing’oa Temeke kwenye nusu fainali iliyochezwa leo (Septemba 13 mwaka huu) asubuhi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam.

Ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa dakika za 30 na 63 kupitia Juma Ali Yusuf ndiyo yaliyoipa Mjini Magharibi tiketi ya kucheza fainali itakayofanyika kesho (Septemba 14 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia saa 9 alasiri.

Mjini Magharibi itacheza fainali hiyo na mshindi wa nusu fainali ya pili inachezwa leo jioni kwenye uwanja huo huo kati ya mabingwa watetezi Morogoro na Ilala.

Kwa upande wa wasichana Ilala imetinga fainali baada ya kuifunga Kinondoni mabao 2-0 katika nusu fainali ya kwanza. Mabao ya washindi yalifungwa dakika ya 27 na Fatuma Bahau wakati Happiness Lazoni alifunga la pili dakika ya 39.

Nusu fainali ya pili kwa wasichana itakuwa kati ya Mwanza na Mbeya.

30 WAITWA KAMBINI TWIGA STARS
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage ameita kambini kikosi cha wachezaji 30, wengi wao wakiwa vijana ikiwa ni mwendelezo wa programu ya kujenga timu hiyo.

Kambi hiyo itakuwa jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 15 hadi 26 mwaka huu. Vijana wengi wamejumuishwa ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kuandaa timu itakayocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20.

Kaijage amesema pamoja na malengo hayo kwa timu ya vijana, bado maana kubwa inabaki kuandaa Twiga Stars iliyo imara kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Amesema Twiga Stars haikabiliwi na mashindano yoyote mwaka huu, hivyo lengo ni kuijenga upya ndiyo maana haichezi michezo ya kimataifa ya kirafiki hadi itakapofika wakati wake.

Utaratibu huo ulianza kuanzia kambi ya Machi mwaka huu, na ndio umezaa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ambayo sasa itashiriki mashindano ya Kombe la Dunia.

Wachezaji walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden, Pwani), Asha Rashid (Mburahati Queens, Dar es Salaam), Belina Julius (Lord Barden, Pwani), Donisia Daniel (Lord Barden, Pwani), Esther Chabruma (Sayari Queens, Dar es Salaam), Eto Mlenzi (JKT, Dar es Salaam) na Evelyn Sekikubo (Mburahati Queens, Dar es Salaam).

Fatuma Bushiri (Simba Queens, Dar es Salaam), Fatuma Hassan (Mburahati Queens, Dar es Salaam), Fatuma Issa (Evergreen, Dar es Salaam), Fatuma Mustafa (Sayari Queens, Dar es Salaam), Fatuma Omari (Sayari Queens, Dar es Salaam), Flora Kayanda (Tanzanite, Dar es Salaam) na Gerwa Lugomba (Umisseta, Kanda ya Ziwa).

Hamisa Athuman (Marsh Academy, Mwanza), Maimuna Hamisi (Airtel Rising Star, Ilala), Maimuna Said (JKT, Dar es Salaam), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens, Dar es Salaam), Mwapewa Mtumwa (Sayari Queens, Dar es Salaam), Pulkeria Charaji (Sayari Queens, Dar es Salaam) na Rehema Abdul (Lord Barden, Pwani).

Sabahi Hashim (Umisseta, Zanzibar), Semeni Abeid (Tanzanite, Dar es Salaam), Sharida Boniface (Makongo Sekondari, Dar es Salaam), Sofia Mwasikili (Sayari Queens, Dar es Salaam), Tatu Idd (Lord Barden, Pwani), Therese Yona (TSC Academy, Mwanza), Vumilia Maarifa (Evergreen, Dar es Salaam), Yulitha Kimbuya (Marsh Academy, Mwanza) na Zena Khamis (Mburahati Queens, Dar es Salaam).  

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU