Azam Media Limited imefanikiwa kukamilisha utaratibu wa
ushirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) utakaowawezesha mashabiki
wa kandanda kote nchini kunufaika kwa kuona michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom kila
mwishoni mwa juma hadi kukamilika kwa nusu ya msimu wa 2013/14 kupitia TBC1 kwa
hisani ya AzamTV.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na
Bodi ya Ligi (Kamati ya Ligi) wameeleza kuunga mkono utaratibu huu makini.
“Baada ya kupata haki za matangazo ya luninga ya Ligi Kuu
ya Vodacom, moja ya shabaha zetu kuu imekuwa ni kuhakikisha kuwa tunafanikiwa
kurusha matangazo yanayokidhi viwango vya kimataifa kwa ubora. Ili kufanikisha
shabaha hiyo tumewekeza vilivyo katika teknolojia ya kisasa ya vifaa vya
matangazo ya nje (Outside Broadcasting) na katika mafunzo kwa watumiaji wa
vifaa hivyo. Ninayo furaha kusema kuwa matayarisho yamekwenda vema kiasi kwamba
tumejikuta tuko tayari kurusha matangazo ya kiwango cha juu kabla hata ya
kuzinduliwa kwa huduma kamili za AzamTV”, alisema Rhys Torrington, Afisa
Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited.
“Kwa kuwa mashabiki wengi kote nchini wanangojea kwa hamu
kubwa kuziona timu wazipendazo, imeonekana ni vema kuanza kuonesha michezo hii
ya Ligi sasa. Kwa kuzingatia hali hiyo, nilifanya mazungumzo na rafiki zetu
pale TBC na kuwaomba iwapo wana uwezo na kuridhia kurusha matangazo yetu ya moja kwa moja bila
ya malipo yoyote kuanzia mwisho wa juma hili hadi kukamilika kwa nusu msimu.
Tulifanikiwa kufikia makubaliano kwa haraka na sasa tunafanyia kazi masuala ya
kiufundi yatakayowezesha kuwa tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi
utakaofanyika Uwanja wa Taifa”, Aliongeza Bw. Torrington.
Mara tu huduma kamili za AzamTV zitakapozinduliwa majuma
machache yajayo, matangazo ya michezo ya Ligi Kuu kwa wigo mpana yatakuwepo pia
kwenye chaneli yake hadi mapumziko ya nusu msimu. Baada ya hapo matangazo ya
Ligi Kuu ya Vodacom yatapatikana kwa wale tu watakaokuwa na visimbuzi (decorders)
vya AzamTV.
0 maoni:
Post a Comment