CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimekuwa na
utaratibu wa kila mwaka kutoa tuzo kwa wanamichezo wanaofanya vizuri na sherehe
za utoaji wa tuzo hizo zimekuwa zikifanyika kati ya miezi ya Mei na Juni.
Hata hivyo mwaka huu tuzo hizo zimechelewa
kufanyika kutokana na sababu mbalimbali, ambazo zipo nje ya uwezo wa Kamati ya
Tuzo, Kamati ya Utendaji ya TASWA, wanachama wa TASWA, wanamichezo husika na wwandishi
wa habari za michezo kwa ujumla wao.
Ndugu zangu ninyi ni mashahidi wa tuzo za miaka miwili
iliyopita, zilivyofana na zikabaki kupigiwa mfano kwa ubora wake.
Lakini mwaka huu, mambo kidogo yalikuwa magumu
kutokana na kampuni ambayo sitaitaja jina, ambayo awali ilituhakikishia
ingedhamini kwa asilimia 100 lakini ilipata
matatizo ya kiuchumi wiki tatu kabla ya tarehe tuliyokuwa tumepanga kufanya
tuzo, hivyo wakatuomba tusogeze mbele huenda mambo yangeimarika.
Kuanzia hapo kila mara wakawa wanatuhakikishia mambo
yatakuwa mazuri, lakini mwezi Agosti mwishoni wakatupa taarifa rasmi kuwa hawatamudu
kudhamini tuzo zetu, hali ambayo ilituchanganya kwa kiasi kikubwa kwani
ingekuwa vigumu sana kupata wadhamini wa ghafla kwa wakati huo.
Hata hivyo kutokana na heshima ambayo TASWA imejijengea
na kuaminika mbele ya jamii kwa kushirikiana na Kamati ya Tuzo, tukaanza
mazungumzo na kampuni mbalimbali na tayari tumepata kampuni mbili za kutusaidia,
huku tukiendelea na juhudi zetu za kupata wadhamini wa kutosha kulingana na
bajeti yetu.
Leo ninayo furaha kuwatangazia kuwa Desemba 20 mwaka
huu, tutafanya Tuzo ya Wanamichezo Bora wa mwaka 2012 katika ukumbi ambao
tutautangaza hivi karibuni na maandalizi yamefikia hatua nzuri sana.
Tumefanya vikao kadhaa cha mwisho kikiwa jana kati ya
Kamati ya Utendaji ya TASWA na Kamati ya Tuzo, tumetafakari athari za kuchelewa
kufanya na zile za kuacha kufanya, tukajiridhisha ni bora tufanye ingawa
tumechelewa, lakini lazima tuwaenzi wanamichezo waliofanya vizuri mwaka
uliopita.
Tunaomba radhi wanamichezo wanaowania tuzo hizo, vyama
mbalimbali vya michezo na wote ambao kwa namna moja au nyingine kuchelewa kwetu
kuliwakwaza, lakini hatukuwa na jinsi yote ni katika kuhakikisha tuzo zetu
zinakuwa bora kama miaka iliyopita.
Tayari majina ya awali ya wanaowania tuzo kwa michezo
mbalimbali tulishayatangaza, ni jukumu sasa la Kamati ya Tuzo kuendelea na
mchakato ili kuhakikisha zinakuwa nzuri zaidi.
0 maoni:
Post a Comment