Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Jeshi la Polisi kuanzia sasa
halitashikilia silaha za washabiki, na badala yake litawazuia kabisa
kuingia viwanjani wakati wa mechi.
Jeshi
la Polisi limekuwa likihifadhi silaha za washabiki wanaokwenda
viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya mechi kumalizika kwa vile
Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) zinakataza silaha viwanjani.
Wikiendi
iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi
lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa washabiki waliokwenda kushuhudia
mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile kati ya JKT Ruvu na Simba.
Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki.
Hivyo,
kwa washabiki wanaomiliki silaha hatawaruhusiwa kabisa kuingia
viwanjani, na badala yake tunawashauri kuzihifadhi huko wanakotoka kabla
ya kufika viwanjani.
Pia
tunatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona mwenzake akiwa na silaha
uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi la Polisi ili
aweze kuchukuliwa hatua.
UAMUZI KAMATI YA MAADILI KUFANYIWA MAPITIO
Shirikisho
liko kwenye hatua za mwisho za mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa
kufanyika tarehe 26/27 Oktoba 2013 hapa jijini Dar es salaam.
Hivi
sasa, wagombea wanasubiri vyombo vya juu vya uamuzi kwa ajili ya kutoa
uamuzi wa mwisho kabla ya kuanza kampeni na hatimaye uchaguzi.
Hata
hivyo, baada ya Kamati ya Maadili kufanya uamuzi dhidi ya kesi nane
zilizowasilishwa mbele yake, Sekretarieti imeona kuwepo kwa ukakasi
katika utekelezaji wa uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa kuna baadhi ya
mambo yanaonekana kuwa na ugumu katika kuyatekeleza.
Sekretarieti
si chombo chenya mamlaka ya kutafsiri uamuzi wa vyombo huru vya
Shirikisho, kazi yake kubwa ni kupokea uamuzi na kuutekeleza, hivyo kwa
kuwa kuna ukakasi huo imeamua kuwasilisha uamuzi huo kwenye Kamati ya
Rufani ya Maadili kwa ajili ya kuufanyia mapitio (revision) na pia kutoa
mwongozo kabla ya kurejesha uamuzi huo kwenye Kamati ya Uchaguzi kwa
ajili ya kuendelea na mchakato.
Sekretarieti
imefanya hivyo kwa lengo la kusaidia wagombea ambao wengi wanaonekana
kuwa njia panda baada ya kupokea uamuzi wa Kamati ya Maadili na kuiuliza
Sekretarieti kuwa inakuwaje Kamati ya Maadili iwaone hawana hatia,
lakini hapo hapo ikubaliane na uamuzi wa kuwaengua, jambo ambalo kwa
kweli limetufanya tukose majibu sahihi na hivyo kuamua kuomba revision
na mwongozo.
Pia
mwongozo utakaotolewa na Kamati ya Rufani ya Maadili utasaidia kuweka
mwelekeo mzuri wa masuala ya Maadili katika siku zijazo.
Miongoni
mwa mambo yanayoonekana kuwa na ukakasi ni kuwaona watu wote ambao kesi
zao ziliwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili hawana hatia, lakini hapo
hapo kukubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi wa kuwaengua baadhi yao
kwa sababu za kinidhamu ikisema haiwezi kuwahukumu mara mbili kwa kuwa
wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi.
Ili
haki itendeke na ionekane inatendeka, Sekretarieti imeona ni vizuri
masuala hayo yakafanyiwa revision (mapitio) na kutolewa mwongozo ili
kuondoa ukakasi uliojitokeza miongoni mwa wagombea, Shirikisho na wadau
na hivyo kujenga hisia kuwa kuna mbinu zimefanyika dhidi ya baadhi ya
wagombea.
Uamuzi
huu haumaaniishi kuwa Sekretarieti inapingana na uamuzi wa Kamati ya
Maadili, bali ni utaratibu wa Sekretarieti kuomba ufafanuzi au mwongozo
kutoka vyombo husika pindi inapotokea ukakasi katika utekelezaji wa
uamuzi wa vyombo vya uamuzi vya Shirikisho.
Sekretarieti
imeshamwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani za Maadili ili aitishe
kikao kwa manajiri ya kufanya mapitio na kutoa mwongozo ambao utasaidia
Shirikisho kuendelea na uchaguzi bila ya ukakasi.
SERIKALI, TAASISI ZAOMBWA KUISAIDIA U20 WANAWAKE
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiomba Serikali, taasisi na kampuni
mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake kwa
vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda kwa mechi ya Kombe la
Dunia dhidi ya Msumbiji.
Timu
hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani Pwani chini ya Kocha
Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza
itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya TFF, Lina Kessy amesema hiki
ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri
katika mashindano hayo.
Ameitaka
jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo haina mdhamini wala
mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya kusubiri ifanye
vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.
Kessy
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake
Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa fursa ya kambi
kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia huduma nyingine
inazopata hapo.
Vilevile
amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutokana na
ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira wa miguu wa wanawake
kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.
“Shukrani
za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao wachezee timu ya Taifa, kwani
wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa wazazi. Pia
tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia
wachezaji wetu,” amesema.
Fainali
za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo
Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza
na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe.
0 maoni:
Post a Comment