Friday, October 4, 2013

SIMBA KUIVAA RUVU SHOOTING VPL

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka huu)  kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10 kamili jioni vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani kuanzia saa 4 asubuhi.

Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu itakayoumana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Coastal Union ikiwa mwenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ndiyo utakaotoa fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya City kuoneshana ujuzi katika kusaka pointi tatu.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Mgambo Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

FDL KUTIMUA VUMBI VIWANJA KUMI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2014/2015) inaendelea wikiendi hii (Jumamosi na Jumapili) kwa kuzikutanisha timu 20 zitakazopambana katika viwanja kumi tofauti.

Jumamosi kutakuwa na mechi kati ya Green Warriors na Friends Rangers (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Kimondo na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi), Mlale JKT na Mkamba Rangers (Uwanja wa Majimaji, Songea) na Kurugenzi dhidi ya Polisi Morogoro (Uwanja wa Wambi, Mafinga).

Polisi Dodoma na Stand United (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Toto Africans na JKT Kanembwa (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mwadui na Polisi Mara (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Polisi Tabora na Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi kati ya African Lyon na Transit Camp (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Villa Squad dhidi ya Polisi Dar es Salaam (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam).


0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU