Tuesday, October 22, 2013

UCHAGUZI TPL BOARD KUFANYIKA IJUMAA

Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) utafanyika Oktoba 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.

SERENGETI BOYS YAALIKWA MICHUANO YA ANOCA
Timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Serengeti Boys) imealikwa kushiriki Olimpiki ya Afrika itakayofanyika Mei mwakani.

Mpira wa miguu ni kati ya michezo 22 itakayoshindaniwa katika mashindano yatakayofanyika Gaborone, Botswana chini ya Kamati za Olimpiki za Afrika (ANOCA).

Kwa mujibu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Tanzania imepewa nafasi ya kushiriki katika michezo hiyo ya Olimpiki kwa Afrika kutokana na kuwa na programu nzuri za vijana hasa chini ya umri wa miaka 17.

Hiyo itakuwa ni michezo ya Pili ya Afrika kwa Olimpiki ambapo ya Kwanza ilifanyika mwaka 2010 jijini Rabat, Morocco.

YANGA,  SIMBA VIWANJANI VPL J5
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi tatu; ambapo Yanga itaikaribisha Rhino Rangers katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Coastal Union inaikaribisha Simba katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.

Tanzania Prisons ambayo imepoteza mechi mbili zilizopita ugenini dhidi ya Ashanti United na Simba inarejea uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine kwa kuikaribisha Kagera Sugar.

Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi moja ya kundi A itakayozikutanisha Tessema na Villa Squad kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

KIINGILIO MECHI YA U20 WANAWAKE 1000/-
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya wanawake chini ya miaka 20 katika ya Tanzania na Msumbiji itakayochezwa Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa sh. 1,000.

Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni, na kiingilio hicho ni kwa ajili ya viti vya rangi ya kijani, bluu na chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000.

Timu ya Msumbiji inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Oktoba 23 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya LAM. Msumbiji yenye msafara wa watu 25 itafikia kwenye hoteli ya Sapphire.
 
RAMBIRAMBI MSIBA WA JIMMY MHANGO
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya klabu ya Ashanti United, Jimmy Mhango kilichotokea jana (Oktoba 21 mwaka huu).

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mhango aliutumikia mpira wa miguu kwa muda mrefu, tangu akiwa mchezaji, kocha na baadaye kiongozi.

Kabla ya kuingia kwenye Bodi ya Ashanti United, enzi za uchezaji wake alichezea timu za Mapinduzi ya Dodoma, Ushirika ya Moshi na Pan African ya Dar es Salaam. Pia aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Ashanti United.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mhango, klabu ya Ashanti United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko yamefanyika leo mchana katika makaburi ya Abeid (Mchikichini) Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Mhango mahali pema peponi. Amina

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU