Bodi
ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia viwanja saba vilivyokuwa
vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za
mpira wa miguu.
Uamuzi
huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika
juzi (Novemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo
mengine kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa
kwanza.
Viwanja
vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika kwanza ili
viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa
yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji), na Uwanja wa
CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo
(dressing rooms) havina hadhi).
Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni
mbovu), Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha
(pitch ni mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia
kutumika kwa ajili ya shule ya awali), Uwanja wa Majimaji mjini Songea
(pitch ni mbovu) na Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu).
Klabu
ambazo timu zake zinatumia viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya
uamuzi huo ambapo ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja
hivyo ili wafanye marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya kuchezea
mechi zao.
Kwa
upande wa ripoti za mechi za VPL; Mbeya City imepigwa faini ya sh.
500,000 na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya
utangulizi walipocheza na Yanga. Pia wanatakiwa kulipa gharama za
uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga baada ya
gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi.
Pia
Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kushambulia
basi la wachezaji wa Tanzania Prisons baada ya mechi dhidi yao, na
kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi.
Coastal
Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki
wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi
msaidizi Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na
kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu.
Beki
wa Coastal Union, Hamad Khamis wa Coastal Union amepigwa faini ya sh.
500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo
hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa
mechi tatu zinazofuata za timu yake.
Mchezaji
Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa
kupiga kelele wakati mgeni rasmi akisalimia timu na kukataa kupeana
mkono na kamishna kwenye mechi dhidi ya Rhino Rangers, hivyo amefungiwa
mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000.
Mtunza
vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu, Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la
ufundi wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya City kwa kosa la kutoa lugha
chafu kwa refa, hivyo suala lake litapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Kocha
Msaidizi wa Oljoro JKT, Fikiri Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na
kufungiwa mechi tatu kwa kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi
yao dhidi ya Ashanti United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin
amepelekwa Kamati ya Maadili kwa kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.
Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar.
Katika
FDL, mchezaji Ally Mtoni wa Villa Squad amepigwa faini y ash. 200,000
na kufungiwa mechi tano. Kosa lake ni kujisaidia haja ndogo golini wakti
wa mechi dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa mjini Mtwara.
Kamishna
Paul Opiyo wa mechi ya FDL kati ya Villa Squad na Transit Camp kwa
kutokuwa makini. Katika ripoti yake ameeleza kuwa Transit Camp
ilichelewa kufika uwanjani, lakini hakusema ilichelewa kwa muda gani.
Kocha
wa Polisi Dar es Salaam, Ngelo Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi
Masi wamepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi tatu kila mmoja
kwa kuongoza kundi la washabiki kumvamia refa wa mechi yao dhidi ya
Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.
Pia
Bodi ya Ligi imeagiza Polisi waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati
waamuzi wanapigwa walikuwepo lakini hawakutoa msaada kwa wakati.
Kocha
wa Friends Rangers, Kheri Mzozo amepigwa faini ya sh. 200,000 na
kufungiwa mechi sita kwa kosa la kumtukana refa na kutishia kuhamamisha
washabiki waingie uwanjani kufanya fujo kwenye mechi dhidi ya Villa
Squad.
Naye
Kocha msaidizi wa timu ya Transit Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya
sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kutoa lugha ya matusi kwa
mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi ya Friends Rangers.
Adhabu
zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha
kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa
Uwanja wa Kambarage ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo
haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili (Novemba 17 mwaka
huu).
FUTURE TAIFA STARS vs TAIFA STARS UWANJANI KARUME
Timu
za Taifa za Future Taifa Stars na Taifa Stars zinacheza kesho (Novemba
13 mwaka huu). Mechi hiyo ya kirafiki itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi
hiyo ni maalumu kwa Benchi la Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na
Kim Poulsen kuangalia wachezaji kumi kutoka Future Taifa Stars
watakaoongezwa katika Taifa Stars tayari kwa mechi ya kirafiki ya
kimataifa itakayochezwa Novemba 19 mwaka huu jijini Arusha.
Watazamaji 300 tu wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini leo
(Novemba 12 mwaka huu). Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni
kipa Ivo Mapunda wa Gor Mahia.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
0 maoni:
Post a Comment