Wednesday, November 13, 2013

GrandMalt yadhamini Uhuru Marathon

Katibu wa kamati ya serikali ya maandalizi ya mbio za Uhuru marathon Tanzania Innocent Melleck Katikati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam juu ya udhamini wa kampuni ya bia nchini Tbl kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha GrandMalt ambapo kimetoa jumla ya shilingi milioni ishirini (20,000,000) kushoto ni mkurugenzi msaidizi wa idara ya habari maelezo Tiganya Vincent na kulia ni meneja masoko wa Tbl Fimbo Butalla.

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha GrandMalt imejitokeza kudhamini mbio ndefu za Uhuru, Uhuru Marathon, kwa kiasi cha Sh milioni 20.
 
Akitangaza udhamini huo jijini Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema, wameona ni vyema kudhamini mbio hizo kwani zina lengo zuri zaidi la kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
 
Kuhusu udhamini huo, Butallah alisema, Sh milioni 13.4 zitatumika kwa ajili ya kutoa zawadi mbalimbali kwa washindi, huku Sh milioni 6.6 zikiwa ni kwa burudani zitakazofanyika siku ya mkesha wa kuamkia mbio hizo.
 
“Ukweli ni kwamba taifa lolote duniani linapigania kuwa na uchumi imara na pasipokuwa na amani hakuna uchumi utakaoweza kukua, hivyo TBL kama kampuni inayotengeza bidhaa za hapa nyumbani imeona ni muhimu kuungana na Watanzania wenzetu wote kuhakikisha kuwa mbio hizi zinafanyika katika hali ya mafanikio makubwa na kuwa za kufana zaidi.
“Nitoe rai pia kwa makampuni ya ndani na nje ya nchi kujitokeza na pia kuendelea kutoa chochote walichonacho ili kufanikisha mbio hizi zenye kubeba dhima ya Taifa letu lakini pia wajitokeze kwa wingi kushiriki mbio hizi.
 
“Kwa zawadi hizi tulizotangaza leo tunaamini zitakuwa kichocheo kwa wakimbiaji wetu kufanya mazoezi ya kutosha ili kuhakikisha fedha hizi zinabaki ndani ya ardhi ya Tanzania,” alisema.
 
Naye Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo ambazo zina nia kubwa ya kutukumbukusha wajibu wetu wa kutunza na kulinda amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
 
Alisema zawadi kwa mshindi wa kwanza inatarajiwa kuwa Sh 1,500,000 kwa wakimbiaji wa kilomita 21 na 42, hii ni kwa upande wa wanawake na wanaume.
 
Mshindi wa pili kwa mbio hizo iwe kwa upande wa wanawake au wanaume kwa kilomita 21 au 42 ataondoka na Sh 800,000 wa tatu Sh 600,000 wanne Sh 300,000 na watano apata Sh 150,000.
 
Mbio hizi zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam hapo Desemba 8, mwaka huu ambapo zitaanzia na kumalizikia katika Viwanja vya Leaders club.
 
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kushiriki mbio hizi, huku wabunge zaidi ya 100 wakiongozwa na Spika Anne Makinda wakiwa wamejisajili kwa ajili ya kushiriki.
 
Mbio hizo zimegawanywa katika makundi makuu manne ambayo ni kilomita 3 kwa ajili ya viongozi, kilomita 5 kwa watu wote na kilomita 21 na 42 ambazo ni maalum kwa wakimbiaji nguli.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU