Makamu wa Rais wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr
Mohamed Garib Bilal akifuatilia kwa umakini mbio za Uhurumarathon kwenye
viwanja vya Leaders Club jijini Dar Es Salaam
kulia ni mratibu wa mbio hizo Innocent Melleck na kushoto ni waziri wa
habari,vijana,utamaduni na michezo Dr Fenela Mukangara.
Makamu wa Rais wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Mohamed Garib Bilal akizungumza jambo na mratibu
wa mbio hizo Innocent Melleck kwenye mashindano ya riadha ya mbio za
uhurumarathon zilizofanyika kwenye viwanja vya leaders Club jijini
Dar Es
Salaam.
umati wa wakimbiaji wa umbali wa km 21 wakianza mbio hizo jijini dar es salaam
MBIO ndefu za Uhuru, Uhuru
Marathon, zilifanyika jana kwa kuanzia na kumalizikia katika Viwanja vya
Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam huku Watanzania na Wakenya wakichuana
vilivyo na kugawana nafasi za ushindi.
Katika mbio za kilomita 42
upande wa wanaume mshindi alikuwa ni Jamini Ikai kutoka Kenya aliyetumia saa
2:33:35, akifuatiwa na Steven Sylvester wa Tanzania akitumia saa 2:42:05,
nafasi ya tatu ilishikwa na Alex Sanka aliyetumia saa 2:44:14 toka Tanzania pia,
akifuatiwa na James Shigela aliyetumia saa 2:47:40 na watano akiwa Getuni
Gumali aliyekimbia saa 2:52:88.
Kwa upande wa wanawake
nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Thabita Kibeti wa Kenya aliyekimbia saa
3:24:50, akifuatiwa na Naumi Jepkosgei wa Kenya pia aliyekimbia saa 3:45:09 na
nafasi ya tatu ilitwaliwa na Banuelia Brighton wa Tanzania aliyekimbia saa
4:05:36.
Katika kilomita 21 upande
wa wanaume nafasi ya kwanza na pili ilienda Kenya pale Elijah Tirop alipokimbia
kwa saa 1:06:12, akifuatiwa na Wilson Tuitoe aliyekimbia saa 1:06:38, watatu
akiwa Eliah Daudi wa Tanzania aliyetumia saa 1:07: 10, Hilary Kepchumba wa
Kenya akishika nafasi ya nne kwa kukimbia saa 1:07: 12 na ya tano ikaenda kwa
Wilbert Peter wa Tanzania aliyetumia saa 1:08:56.
Kwa upande wa wanawake
nafasi ya kwanza ilikamatwa na Jacqueline Juma wa Tanzania aliyekimbia saa
1:15:25:06, Anjela Temu wa Kenya alitwaa nafasi ya pili kwa kukimbia saa
1:16:01:85, Catherine Range wa Tanzania alikimbia saa 1:17:33:82, Mary
Mangegeia aliyekimbia saa 1:18:26:80 na Agnes Chepete akikimbia saa 1:23:21:85
wote hawa kutoka Tanzania.
Washindi wa mbio ndefu kwa
upande wa mbio za kilomita 42 kwa upande wa wanaume na wanawake kila mmoja
aliondoka na Sh milioni 2, kwa upande wa mbio za kilomita 21 kwa wanaume na
wanawake kila mmoja alipata Sh milioni 1.
Mshindi wa pili kilomiita
21 kwa wanaume na wanawake walipata Sh 700,000 huku kilomita 42 wakiondoka na
Sh milioni 1 kwa kila mmoja.
Mshindi wa tatu kilomita
21 kwa wanaume na wanawake kila mmoja alipata Sh 500,000 na kilomita 42 walipata
Sh 600,000 washindi wa nne kwa kilomita 21 na 42 kwa wanawake na wanaume kila
mmoja aliondoka na Sh 300,000 wakati yule aliyeshika nafasi ya tano kwa
kilomita 21 wanawaume alipata Sh 150,000 na kilomita 42 ilikuwa Sh 200,000 huku
walemavu kumi wakipata Sh 100,000.
Akizungumza kabla ya
kukabidhi zawadi Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal alisema,
amefurahishwa mno na wazo la kuanzisha mbio hizo, ambalo ni kulinda na
kudumisha Amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu, huku akionya wale wote
wanaotaka kuleta chokochoko.
“Tanzania imesaidia sana
kupigania uhuru wa nchi mbalimbali, hivyo hatuwezi kukubali eti sisi
tugawanyike vipande hiyo haitakubalika na naamini vijana mnaona, mnasikia na
kuwajua wanaoleta chokochoko hizo,” alisema, huku washiriki wakisimama pia
kuomboleza kifo cha Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Awali, Katibu wa Kamati ya
Mbio hizo, Innocent Melleck alitumia pia fursa hiyo kuiomba Serikali kuwasaidia
zaidi, kwani mwakani wanataka kulisambaza katika mikoa mbalimbali ili kudumisha
umoja wa Kitaifa.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais
mwakani ni miaka 50 ya Muungano tunatarajia kuanza maandalizi mapema na
tutafanya uzinduzi rasmi Butiama mkoani Mara, ikiwa ni kumuenzi Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, kasha tutafanya matamasha kama hayo katika kanda sita
tofauti kabla ya kumalizia kwenye mbio za Uhuru tarehe 8 Desemba jijini Dar es
Salaam, kwa umemwakilisha Mheshimiwa Rais, tunaomba utuwakilishie hili kwake
ili tupate sapoti ya serikali katika jambo hili la kudumisha Amani na umoja wa
kitaifa tuliorithishwa na waasisi wa taifa hili,” alisema Melleck.
Akijibu hilo, Makamu wa
Rais alimwagiza Katibu Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya michezo kuhakikisha
hilo linatekelezeka.
Mbio za Uhuru zilidhaminiwa
na GrandMalt, Konyagi, Kibuku, Mwananchi Communications, Sayona, CocaCola,
KAPARI, Clouds FM, Uhuru FM, TBC 1, TBC Taifa, Integrated Communications, Night
Support, Tindwa Medical, Forever Living na SamSung.
0 maoni:
Post a Comment