Monday, January 13, 2014

MALINZI KUTEMBELEA KITUO CHA ALLIANCE



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atafanya ziara ya siku moja kutembelea kituo cha mpira wa miguu wa vijana cha Alliance cha jijini Mwanza.

Lengo la ziara hiyo ni kuangalia jinsi Alliance inayoendesha shughuli zake ili Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liweze kushirikiana na kituo hicho kwa karibu.

Rais Malinzi katika ziara hiyo atakayoifanya keshokutwa (Januari 15 mwaka huu) atafuatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu kwa Vijana, Ayoub Nyenzi na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ramadhan Nassib.

Alliance inatarajia kufanya mashindano yatakayoshirikisha vituo vyote vya kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana (academy) wiki ya tatu ya Februari mwaka huu jijini Mwanza.

Mashindano hayo yatashirikisha timu za umri wa miaka 13, 15 na 17 ambapo Alliance itagharamia malazi, chakula na usafiri wakati timu hizo zikiwa jijini Mwanza.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI BONIFACE NJOHOLE
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Boniface Njohole kilichotokea jana (Januari 12 mwaka huu) mkoani Morogoro.

Njohole ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi na Mashindano ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) hadi umauti unamkuta anatarajia kuzikwa kesho (Januari 14 mwaka huu) kijijini kwao Mngeta wilayani Ifakara.

Msiba huu ni mkubwa kwa jamii ya mpira wa miguu kwani alitoa mchango akiwa mchezaji, kocha na kiongozi kwa nyakati tofauti, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Njohole, klabu ya Reli na MRFA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

YAHYA KUFUNGA SEMINA YA WAAMUZI, MAKAMISHNA
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Hamad Yahya atakuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa semina ya waamuzi na makamisha.

Semina hiyo ya siku mbili itafungwa kesho (Januari 14 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Waamuzi zaidi ya 100 na makamishna 50 wanashiriki katika semina hiyo. Makamishna hao ni baadhi ya wale wanaosimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Kwa upande wa waamuzi ni wale wa daraja la kwanza (class one) ambao ndiyo wanaochezesha mechi za VPL na FDL.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatarajia kuandaa semina nyingine baadaye mwaka huu kwa makamishna wapya wanaotaka kusimamia mechi za VPL na zile za FDL.

VITAMBUSHO KWA WAANDISHI WA MPIRA WA MIGUU
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa vitambulisho vipya kwa waandishi wa habari za mpira wa miguu kwa ajili ya kuripoti mechi mbalimbali inayoziandaa na kuzisimamia.

Kila chombo cha habari kupitia Mhariri wake au Mhariri wa Michezo kinatakiwa kuwasilisha majina ya waandishi wake kwa barua maalumu ya ofisi pamoja na picha (soft copy) kwa ajili ya vitambulisho hivyo.

Orodha ya majina ya waandishi wakiwemo wapiga picha wanaoombewa vitambulisho hivyo iwekwe kwa umuhimu.

0 maoni:

Post a Comment

WANAOTEMBELEA KWA SIKU