Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inafikia tamati
kesho (Aprili 19 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya
Azam wakikabidhiwa kombe lao Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi
yao dhidi ya JKT Ruvu.
Mechi
zote saba zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ambapo Yanga na Simba zitakuwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mechi ambayo viingilio vyake ni sh. 5,000
kwa viti vya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000
kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Tayari
tiketi zimeanza kuuzwa leo (Aprili 18 mwaka huu) katika vituo saba vya; Shule
ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kariakoo (Kidongo Chekundu), Buguruni Shell,
mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Ubungo OilCom, Dar Live
Mbagala na Uwanja wa Taifa.
Mechi
nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na Ashanti United (Uwanja wa
Jamhuri, Morogoro), Rhino Rangers na Ruvu Shooting (Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Mgambo Shooting (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Oljoro
JKT na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Coastal
Union na Kagera Sugar (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga).
MICHUANO YA BEACH SOCCER KUANZA JUMAPILI
Michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (Beach
Soccer) inazinduliwa rasmi keshokutwa (Aprili 20 mwaka huu) kwenye ufukwe wa
Escape One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam na kushirikisha timu 13.
Uzinduzi huo utaanza saa 5 asubuhi na mechi
zitachezwa hadi saa 11 jioni. Michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza
nchini inashirikisha timu 13 kutoka vyuo mbalimbali vya jijini Dar es Salaam.
Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (AU), Chuo Kikuu
cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam
(TUDARCO), Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es
Salaam (DSJ) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo
cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha
Utawala wa Kodi (ITA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Michuano hiyo itakuwa inachezwa Jumamosi na
Jumapili kwenye fukwe za Escape One na Gorilla Beach iliyopo Kigamboni, Dar es
Salaam.
WAZOEFU TAIFA STARS KUTAJWA KESHO
Wachezaji
wazoefu wa Taifa Stars watakaoungana na wale 16 waliopatikana katika mpango wa
maboresho wa timu hiyo watatangazwa kesho (Aprili 19 mwaka huu) saa 4 asubuhi
kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itapiga kambi kwenye hoteli
ya Kunduchi Beach kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi
itakayochezwa Aprili 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji
waliopatikana katika mpango wa maboresho ya Stars wanatarajiwa kuwasili leo
(Aprili 18 mwaka huu), na kwenda moja kwa moja kambini kuwasubiri wenzao
watakaotajwa kesho (Aprili 19 mwaka huu).
Wachezaji
hao ni kipa Benedicto Tinoko Simwanda (Mara), Emma Namwondo Simwanda (Temeke), Joram
Nason Mgeveje (Iringa), Omari Ally Kindamba (Temeke), Edward Peter Mayunga (Kaskazini
Pemba), Shiraz Abdallah Sozigwa (Ilala), Yusuf Suleiman Mlipili (Temeke) na Said
Juma Ally (Mjini Magharibi).
Wengine
ni Abubakar Ally Mohamed (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magona (Shinyanga),
Omari Athumani Nyenje (Mtwara), Chunga Said Zito (Manyara), Mohammed Seif Saidi
(Kusini Pemba), Ayoub Kasim Lipati
(Ilala), Abdurahman Othman Ally (Mjini
Magharibi) na Paul Michael Bundara (Ilala).
0 maoni:
Post a Comment