Balozi muambata wa utamaduni wa China, Liu Dong akifafanua jambo wakati alipomtembelea Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego (Kulia) ofisini kwake Ilala,Sharif Shamba wiki hii.Katikati ni wakurugenzi idara mbalimbali za BASATA
Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Materego akisisitiza juu ya uimarishaji wa uhusiano wa kitamaduni kati ya China na Tanzania wakati alipopokea ugeni wa maafisa watatu kutoka Ubalozi wa China ukiongozwa Balozi muambata wa utamaduni Bw.Liu.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeingia kweye makubaliano na ubalozi wa China nchini ya kubadilishana kazi za sanaa na wasanii mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha mashirikiano ya kiutamaduni na kukuza sekta hiyo nchini.
Akiwa katika ziara yake BASATA ambayo aliambatana na maofisa wawili wa ubalozi wake Huang Wei na Wang Hong,Balozi muambata wa utamaduni kutoka China,Liu Dong amesema kwamba nchi yake imejipanga kusaidia sekta ya utamaduni nchini kwa kuwashirikisha watanzania kwenye matamasha mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya sekta hiyo.
Bw.Liu alikubaliana kimsingi na BASATA katika kuimarisha mahusiano ya kiutamaduni ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kuwezesha ubadilishanaji wa kazi za sanaa na wasanii ili wapate fursa za kuuza kazi zao, kujitangaza na kushiriki katika matamasha mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
“China kwa sasa inaweka nguvu kwenye suala la kubadilishana utamaduni baina ya mataifa haya mawili.Tunategemea kuwashirikisha wasanii wa Tanzania katika matamasha mbalimbali tutakayoyaandaa pamoja na kuwapeleka nchini China kwa ajili ya kuongeza na kubadilishana ujuzi” alisisitiza Liu huku akitaja sanaa za uchongaji, filamu, uchoraji, ngoma za asili, sarakasi na nyinginezo kuwa watazipa msisitizo.
Kwa kuanzia Balozi huyo wa China alisema kwamba,wasanii wa Tanzania watapata nafasi ya kushiriki matamasha na maonesho ya kuazimisha mwaka wa China ambayo yanatazamiwa kuanza mwishoni mwa Februari mwaka 2011 ambapo pamoja na wasanii kutoka Tanzania watakuwepo pia magwiji wa tasnia hiyo kutoka China pamoja na waandishi wa habari maarufu.
Kwa upande wake,Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba, ziara hiyo ya maofisa wa ubalozi wa China ambayo imekuja baada ya ile ya awali ya maofisa wa Baraza ubalozini kwao ni yenye manufaa makubwa na italeta tija kubwa katika tasnia ya sanaa na utamaduni kwa ujumla hasa ukizingatia wasanii wamekuwa na uhitaji mkubwa wa maonyesho na masoko ya kazi zao.
Alingeza kwamba,BASATA iko tayari kusaidiana na China katika masuala mbalimbali ya ukuzaji wa sekta ya sanaa huku akiweka wazi kwamba,uhusiano wa China na Tanzania ni wa muda mrefu sana hivyo kuna kila sababu ya kuuendeleza na kuuimarisha zaidi.
“Kama kuna suala lolote mtakalohitaji tuwasaidie katika kukuza ushirikiano wa kiutamaduni sisi tuko tayari na milango iko wazi.Bila shaka eneo hili la mashirikiano ya kiutamaduni ni nyeti sana na hatuna budi kulipa msukumo wa kipekee” alisisitiza Materego
0 maoni:
Post a Comment